Tuesday, September 3, 2013

MWENYEKITI WA MTANDAO WA WANAMUZIKI JOHN KITIME, ATEULIWA MJUMBE WA BASATA


Profesa Penina Mlama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Profesa Penina Mlama kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari - MAELEZO leo, Uteuzi huo wa Profesa Mlama unaanzia mwaka 2013 na unatarajia kumalizika mwaka 2016.
Prof. Mlama ni Profesa wa Sanaa na Sanaa za Maonyesho Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara ameteua jumla watu 12 kuwa wajumbe wa BASATA kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka huu.
Walioteuliwa ni pamoja na wawakilishi wa Vyama na Asasi mbalimbali wa Baraza hilo ambao ni Dkt. Vincensia Shule, John Kitime , Angela Ngowi, Dkt. Herbert Makoye, Erick Shigongo na Alex Msama.
John Kitime

Wawakilishi wengine ni pamoja na Juma Adam Bakari, Daniel Ndagala, Michael Kadinde na Joyce Fisoo.
Wanaoingia kwa mujibu wa nyadhifa zao ni Prof. Hermas Mwansoko na Katibu Mtendaji wa BASATA.
Katika hatua nyingine Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara amemteua Bwana Ghonche Materego kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
Kabla ya uteuzi huo Materego alikuwa amemaliza muda wake kama Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa.
Wajumbe wa Bodi hiyo walioteuliwa na Waziri Mukangara ni Dkt. Herbert Makoye, Prof. Emanuel Mbogo, Dkt. Lucy Mboma, Prof. Hermas Mwansoko pamoja na Katibu Mtendaji wa BASATA.
Wakati huo huo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara ameteua jumla ya watu 21 kuwa wajumbe wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.
Wajumbe hao ni Dkt. Shani Omari, Prof. Yohana Msangila, Ester Riwa, Dkt. Issa Zidi, Khadija Juma na Dkt. Martha Qorro.
Wengine ni Mmanga Mjawiri, Razia Yahaya, Richard Mbaruku, Selina Lyimo, Keneth Konga, Amour Khamis, John Kiango, na Shani Kitogo.
Wajumbe wengine ni Ally Kasinge, Ahmed Mzee, Rose Lukindo, Shabani Kisu pamoja na Edwin Mgendera.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo la BAKITA atachaguliwa na wajumbe watakapokutana kwenye kikao chao cha kwanza.

Thursday, August 22, 2013

Mwenyekiti na Mweka Hazina katika mafunzo ya siku tatu

Mwenyekiti wa Mtandao John Kitime na Mweka hazina wa Mtandao Bi Asha Salvador, wamo katika mafunzo ya siku tatu ya Public Policy Advocacy, mafunzo yanayoendelea UDSM

Friday, August 16, 2013

KICHEKESHO..MWANAMUZIKI NA NJAA ZAKE

Mwanamuziki mmoja alikuwa na tabia ya kukuta mkewe kampikia chakula kila alipotoka kazini usiku. Siku moja mkewe akawa anaumwa hakupika hivyo jamaa aliporudi hakukuta chakula akalazimika kulala njaa. Katika usingizi akaota ankula ugali  wa nguvu. Asubuhi alipoamka akakuta katafuna kona nzima ya godoro

Wednesday, August 14, 2013

Sikiliza SIUMWI SIKU YA MSHAHARA ya Soggy The Hunter

Msanii Anselm Soggy The Hunter ametuma kazi yake hii na haya ndio maelezo ya kazi hiyo.......
Ndugu zangu baada ya kuufanyia mixing upya sasa naachia rasmi ngoma yangu mpya SIUMWI SIKU YA MSHAHARA nikiwa na WATENGWA na imetengenezwa ARUSHA chini ya DAZ NALEDGE naombeni msaada wenu.Ni aina ya Hip-hop ngumu ambayo sijawahi kufanya miaka yangu yote miaka 18 kwenye muziki

Wanamuziki wakutana na kusafisha ofisi yao mpya.

 Katika kuonyesha kuwa wako katika nia ya ujio mpya wanamuziki kadhaa walikutanika na kufanya usafi wa ofisi yao asubuhi ya leo. Samani za ofisi zinategemewa kuingizwa siku ya  Alhamisi na baada ya hapo Katibu Mkuu Abraham Kapinga mwanamuziki mpiga gitaa wa Tanzanite Band atatoa ratiba ya matumizi ya ofisi.





Tuesday, August 13, 2013

MKUTANO WA WANAMUZIKI WAFANA


Ule mkutano ulioitishwa na Tanzania Musicians network (TMN) au Mtandao wa Wanamuziki  Tanzania umekuwa wa mafanikio makubwa. Kwanza kwa mahudhurio ya wasanii mbalimbali wakiwemo wanamuziki wa muziki asili, taarab, dansi, bongoflava na gospel, pia kulikuweko na mameneja wa wanamuziki na mabendi mbalimbali, producers. Hii ilikuwa ni mafanikio makubwa kwani ilionyesha maana halisi ya mtandao.
Pamoja na maelezo ya madhumuni ya kutengeneza mtandao, mwenyekiti wa Mtandao John Kitime alieleza kuwa wanamuziki wa Tanzania lazima wafanye kazi ya ziada ili kuwakamata kimaendeleo wenzao wa nchi nyingine Afrika. Wanamuziki walielezwa umuhimu wa kutumia teknolojia ya internet kwa kuhakikisha kuwa kila mwanamuziki ana anwani ya barua pepe na kujitahidi kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na kuitumia vizuri kwa kutangaza kazi zao. Wanamuziki walikaribishwa kutumia blog yao ya www.tanzaniamusicians.blogspot.com kwa kupeleka matangazo, picha za matukio mbalimbali hata ya shughuli binafsi kama birthday, harusi na  kadhalika na pia kutuma hata nyimbo zao ili ziweze kutundikwa katika mtandao huo bure bila malipo. Wanamuziki walielekezwa kutuma kazi zao kupitia anwani ya musicnettz@gmail.com.
Katibu Mkuu wa mtandao Abraham Kapinga, alitoa maelezo kuhusu hali ya ofisi, ambapo wanamuziki walielezwa kuwa ofisi iko Kinondoni karibu na American Chips, mtaa wa CHADEMA, na kwa vile ndio tumekabidhiwa ofisi, wanamuziki waliafikiana kukutana hapo na kuifanyia ofisi usafi, jambo ambalo nalo lilionyesha nia ya wanamuziki kulea chama chao. Mwanamuziki Hussein Jumbe alijitolea viti 4 kwa ajili ya ofisi, jambo ambalo kwa kila hali ni la kutia moyo kuhusu mwanzo huu wa mtandao.
Mweka hazina wa Mtandao Asha Salvador alitoa taarifa ya vifaa vya ofisi vilivyonunuliwa vikiwemo viti, meza feni, na stationary.
Maelezo mengine muhimu yaliyotolewa ni kuhusu wanamuziki kujiunga na chama, na kulipia ada ili kuweza kuendesha ofisi. Fomu za wanachama ni shilingi 1000/- ada ya mwaka 5,000/- na kiingilio ni shilingi 20,000/-.
Wajumbe walipata muda wa kutoa mawazo na mapendekezo. Mjumbe mmoja alitoa mapendekezo ya mtandao kuwezesha wanamuziki kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya  Katiba ya nchi na  mjumbe mmoja alijitolea kufuatilia taratibu za kuhakikisha wanamuziki wanashiriki katika jambo hilo muhimu.  Mjumbe mwingine alitaka Mtandao uandae program za elimu ya Management ya Band na hata elimu kwa wanamuziki kujitambua na hivyo sio kufika mahala kuporomoka baada ya muda mfupi, pia itolewe elimu kuhusu haki mbalimbali za wanamuziki. Mmoja wa wajumbe alieleza kuwa ametoka nje ya nchi karibuni alikopata elimu ya vocal training, na hivyo Mtandao uandae taratibu ili elimu hii iwafikie wanamuziki waimbaji.
Mjumbe mmoja alitoa taadhari kuhusu hali inayoelekea sasa ambayo inafanya kuweko na uhasama kati ya wanamuziki wa kizazi kipya na wale wa zamani, badala ya wote kutambuana kuwa ni wanamuziki wanaoweza kufanya kazi pamoja na kupata mafanikio makubwa zaidi, Mtandao uliombwa uwe chombo cha kuunganisha wanamuziki wote bila kujali aina ya muziki wa rika.
Swala la vyombo vya utangazaji liliongelewa hasa kuhusu rushwa iliyokithiri katika vyombo hivi ikawekwa hadharani. Mjumbe mmoja alieleza kuwa imefikia kuwa inahitajika shilingi milioni moja kuwezesha wimbo kupigwa katika radio, kwani kuna mgao wa kuanzia mtu anaweka nyimbo kwenye playlist hadi watangazaji wa vipindi mbalimbali kwa ajili ya kupiga muziki na interviews. Ilionekana tatizo hilo lipo hata kwenye radio zinazopiga muziki wa Gospel ambako tofauti ni bei tu. Ambapo bei ya kupigwa wimbo ni kati ya shilingi alfu 80 hadi laki moja. Mtandao ulitakiwa ufuatilie utekelezaji wa sheria ya kulipia matumizi ya muziki katika vyombo vya utangazaji, ambayo ilikuwa ianze kutumika toka 2003.
Wanamuziki walimaliza siku kwa kutumia muda kujaza fomu za uanachama.






Sunday, August 11, 2013

MKUTANO WA WANAMUZIKI JUMANNE 13 AGOSTI 2013 BASATA

MTANDAO wa Wanamuziki utakuwa na  mkutano  wa wanamuziki siku ya Jumanne tarehe 13 kuanzia saa 4 hadi saa 6 pale BASATA Ilala Sharif Shamba.kati ya mambo yatakayofanyika ni kuhamasisha uandikishaji wa wanachama wapya, na pili kupata taarifa ya mpango wa Bima ya Afya kwa wanamuziki. Wanamuziki wote na wadau wengine wanaofanya kazi katika tasnia hii ya muziki, wakiwemo pia waalimu wa muziki, producers, wacheza shoo, mameneja na kadhalika

Monday, August 5, 2013

UJUE MTANDAO WA WANAMUZIKI TANZANIA, hali halisi sasa na malengo kwa muda mfupi ujao

TANZANIA MUSICIANS NETWORK ni mkusanyiko ya wadau wote wanaofanya kazi kwa njia moja au nyingine katika tasnia ya muziki. Muziki hapa ukiwa na maana ya mapana yake yote, muziki wa vikundi na ule wa watu mmoja mmoja, na bila kuwa na mipaka ya aina ya muziki na bila kujali kama ni muziki asili au muziki mapokeo, hivyo kila mtu anaefanya kazi ya muziki bila kujali umaarufu wake au aina ya muziki wake anakaribishwa. Chama pia kinakaribishwa watendaji wengine katika muziki kama vile mameneja , maproducer wa audio na video, mafundi mitambo wa studio na wale wa 'live', dancers maarufu kama stageshow, na wachezaji wa ngoma za asili. 
Wanachama wa Mtandao ni watu binafsi na si vikundi.
Mtandao una lengo la kuwakusanya wadau katika tasnia hii kuwa na sauti moja ili kuweza kurekibisha taratibu za utendaji katika tasnia hii na kuwawezesha wahusika wote kupata stahili zao kama inavyotakiwa. Mtandao ni mwanachama hai wa International Federation of Musician na hivyo moja ya malengo ya Shirikisho hilo ni kuhakikisha kazi ya muziki inatambuliwa kama ajira nyingine na hivyo kutungiwa sheria za kazi na taratibu za kazi kama kazi nyingine, na hivyo mtandao nao kulenga kufikisha hali hiyo kwa wanamuziki wa Tanzania. Kwa kipindi hiki cha awali ajenda nyingine kubwa ni kuweza kufanikisha kupatikana kwa Bima za Afya kwa wanamuziki wanachama mazungumzo yamekwisha anza na vyombo husika ili hili liwe limeanza kutekelezwa kabla ya mwisho wa mwaka.
Kwa wakati huu Mtandao uko chini ya uongozi wa muda 
Mwenyekiti:  John Kitime -Mwanamuziki Kilimanjaro Band
Katibu Mkuu: Abraham kapinga- Mwanamuziki Tanzanite band
Mweka Hazina: Asha Salvador- mwanamuziki Hisia Sound
Mpaka sasa kuna kamati mbili, zenye wanamuziki mchakanyiko vijana na wakongwe, ambazo ziko kazini
i. kamati ya utawala ambayo imewezesha kupatikana kwa ofisi na baadhi ya vifaa vyake na sasa inaanza taratibu za uandikishaji wa wanachama
ii. kamati ya fedha ambayo inaratibu mapato na matumizi ya fedha.
Kamati ya tatu itaanza kazi kabla ya tarehe 15 mwezi huu ambayo itashughulikia na utayarishaji wa ripoti ya hali halisi ya shughuli za Hakimiliki, jambo ambalo litahusisha researchers wa ndani na nje ya nchi, workshop kubwa ya wanamuziki mwezi wa tisa, na hatimae shughuli nzima kutoa ripoti ambayo itaweza kutumika na vyombo mbalimbali vinavyohusika na muziki na ripoti itasaidia sana Serikali kuanza kutoa maamuzi sahihi.

Sunday, August 4, 2013

MASHUJAA BAND YATAMBULISHA NYIMBO ZAKE ITAKAZO REKODI


Jana Jumamosi  tarehe 3 Agosti, bendi ya Mashujaa ilifanya jambo ambalo ni nadra kufanyika katika bendi siku hizi. Bendi hii ilialika wadau na wapenzi wa bendi ili waweze kuzisikiliza nyimbo ambazo bendi hii inatarajia kuzirekodi. Bendi ilipiga mfululizo wa nyimbo  tano, zilizokuwa katika miondoko mbalimbali . Kwa ujumla bendi ina waimbaji wazuri sana kadri ya mazingira ya uimbaji wa siku hizi. Nyimbo zilikuwa nzuri japo zingeweza kuwa bora zaidi kwa kuongeza effects katika magitaa, na urekibishaji wa sauti  kwa ujumla(maarufu kama setting) , japo ungeboreshwa zaidi. Tatizo la setting ya vyombo kwa ujumla limekuwa sugu kwa bendi nyingi, kiasi kuwa kama ni kawaida kukuta sauti zikitoka kwa kikwaruzo na mara nyingine kutosikia waimbaji wanatamka nini katika wimbo.
Album hii itakuwa na mvuto kwa wapenzi wa muziki wa sebene, na pia ni album ya kwanza baada ya bendi hii kubeba tuzo tano katika Kili Music Awards karibuni.
Kati ya wadau waliokuweko katika shughuli hii ni wakali kama deo mwanatanga, William kaijage, Mafumu Bilali, Khalid Chokoraa, Khamis Dacota, John Kitime na wengine wengi walitoa mawazo yao kila baada ya wimbo kwisha ni jambo zuri kama litaendelezwa na pia kama litachukuliwa kwa uzito unaostahili na wanamuziki kwa upande wao.






Saturday, August 3, 2013

TAAARIFA YA MSIBA--AGE KAUZENI HATUNAE TENA

Mwanamuziki wa zamani wa Biashara Jazz Band na JUWATA Jazz Band Agae Kauzeni hatunae tena. Kwa maelezo ya Mwanamuziki Bonzo Kwembe, marehemu amekuwa anaugua kwa kipindi cha mwezi mmoja.Agai amefariki leo Visiga Kibaha. Na mipango ya mazishi inafanyika ili mazishi yawe kesho Kibaha Mnemera. Mungu Amlaze pema peponi

Wednesday, July 31, 2013

DIAMOND MUSICA ORIGINAL WAKIWA KAZINI

KIONGOZI WA BENDI




MWENYEKITI NA MWEKA HAZINA WA TANZANIA MUSICIANS NETWORK WAKITIA SAINI MAKUBALIANO YA UTAFITI KUHUSU HALI YA MUZIKI TANZANIA

BEST AC imeuwezesha Mtandao wa muziki Tanzania kufanya utafiti wa kina na kisha kuja na majibu ya matatizo ya wanamuziki wa Tanzania hasa katika swala la Hakimiliki. Katika makubaliano hayo Mtandao utapata dola 49,000, zitakazolazimika kupatikana kwa ripoti katika muda wa miezi mitatu ijayo
Hans muwakilishi wa BEST AC

Mwenyekiti wa Mtandao John Kitime akitia sahihi makubaliano hayo kwa niaba ya Mtandao

Asha Warsama Salvador Mweka hazina akitia sahihi kwa niaba ya Mtandao

SIKILIZA KIBAO KIPYA CHA DIAMOND MUSICA ORIGINAL- HATUA

KIKAO CHA MUHIMU CHA WANAMUZIKI CHAFANYIKA BASATA LEO







Wanamuziki chini ya chombo chao kipya Tanzania Musicians Network (Mtandao wa Wanamuziki Tanzania) leo wamekutana katika ukumbi wa BASATA na kufanya mkutano amba katika mkutano huo wameongelea mambo muhimu yafuatayo;
 Mwenyekiti wa Mtandao John Kitime aliwaeleza hali halisi ya Mtandao ambao kwa kipindi hiki umejipanga kufanya kazi kadhaa baada ya kulipa ada zake zote BASATA na hivyo kuwa halali wameweza kuingia katika makubaliano na BEST AC ambapo Mtandao utapewa Dola 49,000 USD, katika awamu tatu, ili kuweza kufanya utafiti wa tatizo linalokabili sekta ya muziki Tanzania hasa katika nyanja ya Hakimiliki. Fedha hizi ni zamradi ambao utachukua miezi mitatu ambapo mtafiti au watafiti watafanya research ya kutafuta nini chanzo cha matatizo ya hakimiliki katika tasnia ya muziki, na pia kifanyike nini, na ripoti ipatikane ya kuuuwezesha Mtandao kuongea na wadau wengine katika muziki , ikiwemo serikali, vyombo vya utangazaji, vyombo vingine kama BASATA, TCRA, COSOTA na kadhalika ili kuwezesha wanamuziki wa Tanzania wanufaike na kazi zao. Pamoja na ripoti hiyo kutakuweko na semina kubwa ya wanamuziki kuboresha ripoti hiyo na hatimae kuweza kuwa na mkutano wa wanamuziki na wadau waliotajwa hapo juu. Pamoja na hayo yote Mtandao utatengeneza vipindi kadhaa vya redio vitakavyoanza kurushwa karibuni ambavyo vitayaweka wazi mazingira yaliyomo katika tasnia hii na namna ya kuyakabiri.
Pamoja na maelezo hayo wanamuziki walitaarifiwa kuwa Mtandao umepata ofisi katika maeneo ya Kinondoni jirani na American Chips katika mtaa yalipo Makao Makuu ya CHADEMA. Kodi ya ofisi imekwisha lipia na baadhi ya samani zimenunuliwa, japo wanamuziki waliombwa kama wana samani yoyote wanayoweza kujitolea itapokelewa kwa mikono miwili.
Wanamuziki walitaarifiwa kuwa kupatikana kwa ofisi kutarahisisha uandikishaji wa wanachama wapya. Malipo ya wanachama yapo kama ifuatavyo.
Fomu za uanachama- 1000/-
Kiingilio - 20,000/-
Ada -5,000/- kwa mwaka, fomu zitaanza kupatikana JUmatatu ijayo katika ofisi mpya ya chama.
Wanachama walitaarifiwa kuwa anwani ya email ya cham ni musicnettz@gmail.com na blog hii ilitambulishwa. Wanamuziki waliombwa kuitumia blog hii kama gazeti lao la kuelezea shughuli zao zote bila kuwa na woga.


Tuesday, July 30, 2013

MKUTANO WA WANAMUZIKI WOTE BASATA

Mkutano wa wanamuziki kuweko Jumatano tarehe 31 July 2013, BASATA, kuanzia saa nne hadi saa sita. Katika mkutano huo ajenda kubwa itakuwa kutambulisha Mtandao upya kwa wanamuziki na kupeabna taarifa za hali halisi, na kisha kupeana majukumu, wanamuziki wa kila aina aina ya muziki tunakaribishwa.

Thursday, July 25, 2013

MWANAMUZIKI WA ZIMBABWE CHIWONISO MARAILE AFARIKI DUNIA

Mwanamuziki Chiwoniso Maraile wa Zimbabwe amefariki dunia baada ya kuugua kwa matatizo ya mapafu. Chiwoniso ambaye amewahi kuja Tanzania na kurekodi katika studio za Marimba Studio akifanya kazi na wanamuziki wa hapa nchini kama Karola Kinasha, Norma Bikaka, Bob Rudala, alikuwa mahiri sana kwa chombo chake cha Mbira na kuimba pia.
Mungu amlaze pema mwenzetu

Tuesday, May 28, 2013

SOMA GAZETI LA INTERNATIONAL FEDERATION OF MUSICIANS HAPA

INGIA HAPA KUSOMA GAZETI LA INTERNATIONAL FEDERATION OF MUSICIAN BONYEZA

Tanzania Musicians Network chaanza upya kwa kishindo

-->
Tanzania Musicians Network au Mtandao wa  Wanamuziki Tanzania ni chombo kilichosajiliwa BASATA  2004, kilianza kwa nguvu mwaka 2006 na kufikia kuwa na wanachama 400, lakini  kilipata pigo mwaka 2007 kwa jengo ambalo lilikuwa ofisi ya chama hiki kuvunjwa na kulibadilishwa matumizi na mwenye mali, cham kikadorora.
Kutokana na umuhimu wa chombo hiki na kutokana na pengo la chombo chenye kukusanya wanamuziki wote na washiriki wengine kwenye muziki, wakiwemo, wanamuziki, wachezaji( stage show), sound engineers wa studio na wa muziki ‘live’, producers, managers na wadau wengine wa aina hiyo, imelazimika kukifufua tena chombo hiki muhimu.  Lengo kuu la mtandao huu ni kuwa chama cha wafanyakazi wanamuziki (Musicians Union). Chombo chenye kulea na kukuza shughuli hii kuwa yenye taratibu zinazompasa mfanya kazi wa kazi hizi, kama inavyokuwa katika ulimwengu sehemu nyingine.Chombo hiki ni mwanachama hai wa Shirikisho la Wanamuziki Duniani (FIM).
Kwa sasa ajenda iliyo mbele ni bima ya afya ya wanamuziki. Si siri kuwa tatizo la matunzo na huduma za wanamuziki na wafanyakazi wengine wa tasnia hii ni gumu pale afya zao zinapokuwa na matatizo, hivyo tayari viongozi wameshakuwa na mazungumzo ya awali na moja ya vyombo vya bima ya afya na kinachosubiriwa ni wanamuziki kujiunga na chombo hiki ili kuweza kuanzisha taratibu hizi.
Pamoja na malengo haya Mtandao huu utaendesha semina na warsha kwa ajili ya wanamuziki wanachama katika Nyanja mbalimbali za mambo ya muziki. Katika kipindi hiki hiki tayari mtandao umewezesha wafadhili kufadhili utafiti kuhusu matatizo yaliyomo katika biashara ya muziki jambo ambalo litawezesha wafadhili kufadhili miradi itakayobuniwa katika kurekibisha hali hiyo ngumu.
Tunakaribisha maombi ya uwanachama, unaweza kuonyesha nia kwa kutuma jina na anwani yako katika inbox ya ukurasa facebook Wanamuziki wa Tanzania au kupitia anwani ya musicnettz@yahoo.com na utaweza kuwapewa maelezo ya ziada. Tuma jina lao, jinsia, mahala uliko, namba ya simu, anwani ya email na taaluma unayoshiriki, …. UMOJA NI NGUVU