Tuesday, August 13, 2013

MKUTANO WA WANAMUZIKI WAFANA


Ule mkutano ulioitishwa na Tanzania Musicians network (TMN) au Mtandao wa Wanamuziki  Tanzania umekuwa wa mafanikio makubwa. Kwanza kwa mahudhurio ya wasanii mbalimbali wakiwemo wanamuziki wa muziki asili, taarab, dansi, bongoflava na gospel, pia kulikuweko na mameneja wa wanamuziki na mabendi mbalimbali, producers. Hii ilikuwa ni mafanikio makubwa kwani ilionyesha maana halisi ya mtandao.
Pamoja na maelezo ya madhumuni ya kutengeneza mtandao, mwenyekiti wa Mtandao John Kitime alieleza kuwa wanamuziki wa Tanzania lazima wafanye kazi ya ziada ili kuwakamata kimaendeleo wenzao wa nchi nyingine Afrika. Wanamuziki walielezwa umuhimu wa kutumia teknolojia ya internet kwa kuhakikisha kuwa kila mwanamuziki ana anwani ya barua pepe na kujitahidi kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na kuitumia vizuri kwa kutangaza kazi zao. Wanamuziki walikaribishwa kutumia blog yao ya www.tanzaniamusicians.blogspot.com kwa kupeleka matangazo, picha za matukio mbalimbali hata ya shughuli binafsi kama birthday, harusi na  kadhalika na pia kutuma hata nyimbo zao ili ziweze kutundikwa katika mtandao huo bure bila malipo. Wanamuziki walielekezwa kutuma kazi zao kupitia anwani ya musicnettz@gmail.com.
Katibu Mkuu wa mtandao Abraham Kapinga, alitoa maelezo kuhusu hali ya ofisi, ambapo wanamuziki walielezwa kuwa ofisi iko Kinondoni karibu na American Chips, mtaa wa CHADEMA, na kwa vile ndio tumekabidhiwa ofisi, wanamuziki waliafikiana kukutana hapo na kuifanyia ofisi usafi, jambo ambalo nalo lilionyesha nia ya wanamuziki kulea chama chao. Mwanamuziki Hussein Jumbe alijitolea viti 4 kwa ajili ya ofisi, jambo ambalo kwa kila hali ni la kutia moyo kuhusu mwanzo huu wa mtandao.
Mweka hazina wa Mtandao Asha Salvador alitoa taarifa ya vifaa vya ofisi vilivyonunuliwa vikiwemo viti, meza feni, na stationary.
Maelezo mengine muhimu yaliyotolewa ni kuhusu wanamuziki kujiunga na chama, na kulipia ada ili kuweza kuendesha ofisi. Fomu za wanachama ni shilingi 1000/- ada ya mwaka 5,000/- na kiingilio ni shilingi 20,000/-.
Wajumbe walipata muda wa kutoa mawazo na mapendekezo. Mjumbe mmoja alitoa mapendekezo ya mtandao kuwezesha wanamuziki kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya  Katiba ya nchi na  mjumbe mmoja alijitolea kufuatilia taratibu za kuhakikisha wanamuziki wanashiriki katika jambo hilo muhimu.  Mjumbe mwingine alitaka Mtandao uandae program za elimu ya Management ya Band na hata elimu kwa wanamuziki kujitambua na hivyo sio kufika mahala kuporomoka baada ya muda mfupi, pia itolewe elimu kuhusu haki mbalimbali za wanamuziki. Mmoja wa wajumbe alieleza kuwa ametoka nje ya nchi karibuni alikopata elimu ya vocal training, na hivyo Mtandao uandae taratibu ili elimu hii iwafikie wanamuziki waimbaji.
Mjumbe mmoja alitoa taadhari kuhusu hali inayoelekea sasa ambayo inafanya kuweko na uhasama kati ya wanamuziki wa kizazi kipya na wale wa zamani, badala ya wote kutambuana kuwa ni wanamuziki wanaoweza kufanya kazi pamoja na kupata mafanikio makubwa zaidi, Mtandao uliombwa uwe chombo cha kuunganisha wanamuziki wote bila kujali aina ya muziki wa rika.
Swala la vyombo vya utangazaji liliongelewa hasa kuhusu rushwa iliyokithiri katika vyombo hivi ikawekwa hadharani. Mjumbe mmoja alieleza kuwa imefikia kuwa inahitajika shilingi milioni moja kuwezesha wimbo kupigwa katika radio, kwani kuna mgao wa kuanzia mtu anaweka nyimbo kwenye playlist hadi watangazaji wa vipindi mbalimbali kwa ajili ya kupiga muziki na interviews. Ilionekana tatizo hilo lipo hata kwenye radio zinazopiga muziki wa Gospel ambako tofauti ni bei tu. Ambapo bei ya kupigwa wimbo ni kati ya shilingi alfu 80 hadi laki moja. Mtandao ulitakiwa ufuatilie utekelezaji wa sheria ya kulipia matumizi ya muziki katika vyombo vya utangazaji, ambayo ilikuwa ianze kutumika toka 2003.
Wanamuziki walimaliza siku kwa kutumia muda kujaza fomu za uanachama.






No comments:

Post a Comment