Friday, October 21, 2016

MZEE KUNGUBAYA AZIKWA NA WENGI

MWANAMUZIKI mkongwe ambaye alipata umaarufu kutokana na wimbo wake Salam za Wagonjwa amezikwa leo katika makaburi ya kifamilia Njeteni Kwembe. Msiba huo ulihudhuria na watu wengi wakiwemo majirani, ndugu, wanamuziki na wapenzi wa muziki wa Mzee Kungubaya.Tatu itakuwa siku ya Jumamosi 22/10/2016.
Jeneza likiwa nje ya nyumba ya marehemu

Mwanamuziki Mjusi Shemboza akiongea na mmoja wa watoto wa marehemu Mzee Kungubaya




Mjusi Shemboza akiwa na Mtendaji Mkuu wa COSOTA wa zamani Mzee Mtetewaunga

Msafara wa kuelekea makaburini



Mazishi ya Mzee Kungubaya

Thursday, October 20, 2016

MZEE OMARI KUNGUBAYA HATUNAE TENA

kungubaya
Mzee Omari Kungubaya akipiga gitaa siku ya mkesha wa msiba wa Dr. Remmy Ongala
MZEE Omari Kungubaya ambaye atakumbukwa kwa wimbo wake Salam za wagonjwa, wimbo uliokuwa ukiashiria kuanza na kuisha kwa kipindi cha salamu za wagonjwa kupitia Radio Tanzania kwa miaka mingi amefariki leo mchana baada ya afya yake kuwa si nzuri kwa muda mrefu. Msiba wake uko nyumbani kwake Njeteni, Mbezi ya Kimara Habari zaidi tutawaleteeni Mungu amlaze pema peponi

Thursday, October 13, 2016

NGUZA VIKING, PAPII KOCHA NA TWANGA PEPETA JUKWAA LA TAMASHA LA WAFUNGWA


Bendi ya African Stars, maarufu kwa jina la Twanga Pepeta kesho itashiriki katika Tamasha la Wafungwa ambalo litaanza saa 2 asubuhi. Katika mambo ambayo yatakuwa makubwa kimuziki ni kushiriki kwa mwanamuziki mkongwe  Nguza Viking na mwanae Papii Kocha ambao kwa sasa wanatumikia kifungo cha maish katika gereza la Ukonga. Pia katika tamasha hilo atakuweko msanii nyita wa muziki wa Singeli Msaga Sumu. Lengo la tamasha hilo ni kuwatia moyo wafungwa na kuwaonyesha kuwa wapo pamoja na Watanzania wenzao walio nje ya magereza. Eric Shigongo Mkurugenzi mkuu wa Global Publishersambao ndio walioandaa tamasha amesema hii ni mara ya pili kuandaa tamasha la namna hii, ambalo lengo ni kunyanyua ari ya wafungwa. Wafungwa waliohudhuria tamasha lililopita ambao walikwisha maliza kifungo wamesifu na kusema tamasha lililopita liliwapa faraja sana. Mratibu wa tamasha hilo Juma Mbizo, amesema mbali na burudani kali kutoka kwa Twanga, kutakuwepo na michezo mbalimbali kama ya mpira wa miguu, kuvuta kamba na mingineyo ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi.  Pamoja na maneno mazuri ya kutia moyo yatakayotolewa na Eric Shigongo, Mkuu wa Gereza la Ukonga, ACP Stephen Mwaisabila naye anatarajiwa kutoa neno katika tamasha hilo sanjari na viongozi wengine wa Jeshi la Magereza.

Saturday, October 8, 2016

RATIBA YA MSIBA WA MAREHEMU SALOME KIWAYA


Taarifa ya ratiba ya msiba wa marehemu Salome Kiwaya aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma na mwanamuziki, aliyefariki jana 07/10/2016, kwa ajali ya gari maeneo ya Kilimo Kwanza Dodoma Mjini. Msiba uko nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Image, Kata ya Kilimani, Wilaya ya Dodoma Mjini. RATIBA:
 1.Tarehe 08/10/2016 - maombolezo  yanaendelea nyumbani Image Kilimani Dodoma.
2.Tarehe 09/10/2016 kuanzia saa 2:00 asubuhi - mwili wa marehemu utaletwa nyumbani kutoka  chumba cha maiti cha General Hospital Dodoma.
3. Tarehe 09/10/2016 saa kuanzia 6:00 mchana -salamu mbalimbali za Viongozi na Makundi Maalumu zitaanza kutolewa.
Saa 8: 00 mchana- mwili wa marehemu utatolewa nyumbani, na kuelekea Kanisa Kuu Roman Catholic. Baada ya Misa, msafara wa mwili wa marehemu utaelekea Kijiji cha Mtila, Kata ya Matola Mkoa wa Njombe kwa ajili ya maziko tarehe 10/10/2016 siku ya Jumatatu.


Friday, October 7, 2016

RIP SALOME KIWAYA


Picha iliyopigwa Uingereza wakati Salome alipoenda huko na Shikamoo Jazz Band. Toka Kushoto Marehemu Salome Kiwaya, Marehemu Papa Wemba, na Marehemu Bi Kidude Mungu awalaze pema.
Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa za msiba wa Mama Salome Kiwaya, mwanamuziki mkongwe. Taarifa zilinifikia kuwa Salome amefariki katika ajali ya gari iliyotokea Dodoma sehemu za Meriwa. Nilimfahamu Salome kwa mara ya kwanza mwaka 1987, wakati nikiwa bendi ya Tancut Almasi Orchestra, tulipopiga kambi Dodoma Hotel kwa muda wa miezi mitatu, tukitoa burudani kwanza kwa wajumbe wa mkutano wa Kizota, kisha wenyeji wa mji wa Dodoma. Katika kufahamiana  kipindi hicho, tuliweza hata  kupiga wimbo wake mmoja ulioitwa Tuhina, uliokuwa ukiimbwa na Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, ambao nao ni marehemu. Siku moja nilipita mtaani Dodoma na kununua kanda za muziki wa Salome, nilizipenda sana nyimbo zake na nikamuahidi kuwa ningejitahidi kuzipeleka kwa watu wenye uwezo wa kuendeleza kazi zile. Nilizipeleka kanda kwa Ronnie Graham, Mscotch mmoja mwenye upenzi na uelewa mkubwa wa muziki wa Kiafrika na hasa rumba, na huyu Mscotch ndie aliyewezesha kuanzishwa kwa bendi ya Shikamoo Jazz Band. Baada ya kuzisikia nyimbo zile akaamua kuwa Salome asindikizane na bendi ya Shikamoo kwenye ziara yao ya Uingereza kama muimbaji wa kike. Salome alienda Uingereza na aliporudi ndipo alipoanza kununa vyombo na kuunda kundi la Saki Stars, ikiwa ni kifupi cha Salome Kiwaya Stars. Mume wake Mzee Kiwaya nae ni msanii maarufu aliyekuwa kiongozi wa kikundi cha Utamaduni cha CDA miaka hiyo ya 80. Kuanzia hapo nimekuwa karibu sana na Salome, miaka ya 90 wakati nikiwa Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Salome ndie alikuwa mwenyekiti wa chama hicho katika mkoa wa Dodoma baada ya mkutano mkubwa wa wanamuziki uliofanyika mwezi June 1998, kule Bagamoyo, ambapo wanamuziki 265 waliweza kukusanyika pamoja na kukaa siku nne katika mji wa Bagamoyo wakifanya warsha za fani mbalimbali za muziki. Katika miaka ya karibuni Salome alishughulika na sanaa ya urembo akiwa wakala wa Miss Tanzania kwa kanda ya Kati na kuweza kutoa MIss Tanzania mmoja, baadae aliingia katika siasa na kufikia kuwa Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Dodoma, lakini aliendelea na muziki katika maisha yake yote.

Mungu Amlaze Pema Salome Kwaya. Ucheshi wako hatutausahau. 
JOHN KITIME