Thursday, November 23, 2017

MTANDAO WA MUZIKI WAMPONGEZA MSAMA

Msama

Kitime
Mtandao wa Muziki Tanzania  umempa hongera  Msama na kampuni yake ya Msama Auction Mart
 kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiendelea nayo muda mrefu ya kukamata wezi wa kazi za muziki na hivyo kutoa mchango mkubwa katika kupunguza uharamia na kuhamasisha uchangiaji wa pato la Taifa kupitia kazi za sanaa. Katika pongezi hizo Mwenye kiti wa Tanzania Musicians Network , John Kitime amesema'Kwa niaba ya wanachama wa chama chetu Tanzania Musicians Network, naomba nitoe shukrani kwa mchango wako mkubwa ambao kampuni yako inaufanya katika jitihada za kupunguza uharamia wa kazi za sanaa Dar es Salaam.  Tuko tayari kushirikiana nawe kila wakati kwa lengo la kuboresha mazingira yanayohusu uboreshwaji wa stahiki za wanamuziki wakati wowote.Tunarudia tena kushukuru kwa hili'
Msama amekuwa akifanya kazi hii ya kukamata kazi zisizo halali kwa miaka mingi, na Kitime amekuwa mwanaharakati wa swala la Hakimiliki kwa miaka mingi pia.

Friday, November 10, 2017

SHIRIKISHO LA MUZIKI TANZANIA LAJIANDA KUTENGENEZA DATABASE YA WANAMUZIKI TANZANIA


Shirikisho la Muziki Tanzania ambalo ni muungano wa vyama vya muziki, jana 9/11/2017,  lilifanya warsha ya kuchambua makubaliano na kampuni ya COGSNET Technologies Ltd ili kuweka mazingira ya kuingia mkataba na kampuni hiyo kwa shughuli ya kuunda Database ya wanamuziki Tanzania.
Mkakati huo ambao ulibuniwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Mwakyembe mwezi mmoja uliopita,  uliongozwa na Rais wa Shirikisho hilo Addo November na Katibu Mkuu John Kitime na hatimae kuweza kufikia hatua ya kukutanisha viongozi wa vyama vyote na kukubaliana umuhimu wa kazi hiyo. Uchambuzi ulichukua zaidi ya saa 7 ambapo wawakilishi 32 kutoka vyama vya muziki 6 walishiriki. Vyama hivyo vilikuwa Chama cha Muziki wa Injili (CHAMUITA), Chama cha Muziki wa Dansi (CHAMUDATA), Chama cha muziki wa Kizazi kipya (TUMA), Chama cha muziki wa rumba (CHAMRUTA), Chama cha Muziki wa Disco (TDMA), Chama cha Madansa (TDA).
 Viongozi wa vyama hivi kwa pamoja walichambua makabrasha mbalimbali yatakayowezesha Shirikisho kuingia mkataba wa kuanza kupata idadi na taarifa kamili za wanamuziki na kazi zao nchini Tanzania. Zoezi hili litakapoanza litafanyika nchi nzima na wanamuziki wa aina zote wataingizwa katika Database na hivyo kutoa picha halisi ya shughuli za muziki nchini na pia kusaidia wanamuziki katika namna mbalimbali ikiwemo kuwarahisishia biashara ya kazi zao.




Viongozi wa vyama mbalimbali vya muziki


Viongozi na wanachama wa vyama vya muziki