Thursday, August 22, 2013

Mwenyekiti na Mweka Hazina katika mafunzo ya siku tatu

Mwenyekiti wa Mtandao John Kitime na Mweka hazina wa Mtandao Bi Asha Salvador, wamo katika mafunzo ya siku tatu ya Public Policy Advocacy, mafunzo yanayoendelea UDSM

Friday, August 16, 2013

KICHEKESHO..MWANAMUZIKI NA NJAA ZAKE

Mwanamuziki mmoja alikuwa na tabia ya kukuta mkewe kampikia chakula kila alipotoka kazini usiku. Siku moja mkewe akawa anaumwa hakupika hivyo jamaa aliporudi hakukuta chakula akalazimika kulala njaa. Katika usingizi akaota ankula ugali  wa nguvu. Asubuhi alipoamka akakuta katafuna kona nzima ya godoro

Wednesday, August 14, 2013

Sikiliza SIUMWI SIKU YA MSHAHARA ya Soggy The Hunter

Msanii Anselm Soggy The Hunter ametuma kazi yake hii na haya ndio maelezo ya kazi hiyo.......
Ndugu zangu baada ya kuufanyia mixing upya sasa naachia rasmi ngoma yangu mpya SIUMWI SIKU YA MSHAHARA nikiwa na WATENGWA na imetengenezwa ARUSHA chini ya DAZ NALEDGE naombeni msaada wenu.Ni aina ya Hip-hop ngumu ambayo sijawahi kufanya miaka yangu yote miaka 18 kwenye muziki

Wanamuziki wakutana na kusafisha ofisi yao mpya.

 Katika kuonyesha kuwa wako katika nia ya ujio mpya wanamuziki kadhaa walikutanika na kufanya usafi wa ofisi yao asubuhi ya leo. Samani za ofisi zinategemewa kuingizwa siku ya  Alhamisi na baada ya hapo Katibu Mkuu Abraham Kapinga mwanamuziki mpiga gitaa wa Tanzanite Band atatoa ratiba ya matumizi ya ofisi.





Tuesday, August 13, 2013

MKUTANO WA WANAMUZIKI WAFANA


Ule mkutano ulioitishwa na Tanzania Musicians network (TMN) au Mtandao wa Wanamuziki  Tanzania umekuwa wa mafanikio makubwa. Kwanza kwa mahudhurio ya wasanii mbalimbali wakiwemo wanamuziki wa muziki asili, taarab, dansi, bongoflava na gospel, pia kulikuweko na mameneja wa wanamuziki na mabendi mbalimbali, producers. Hii ilikuwa ni mafanikio makubwa kwani ilionyesha maana halisi ya mtandao.
Pamoja na maelezo ya madhumuni ya kutengeneza mtandao, mwenyekiti wa Mtandao John Kitime alieleza kuwa wanamuziki wa Tanzania lazima wafanye kazi ya ziada ili kuwakamata kimaendeleo wenzao wa nchi nyingine Afrika. Wanamuziki walielezwa umuhimu wa kutumia teknolojia ya internet kwa kuhakikisha kuwa kila mwanamuziki ana anwani ya barua pepe na kujitahidi kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na kuitumia vizuri kwa kutangaza kazi zao. Wanamuziki walikaribishwa kutumia blog yao ya www.tanzaniamusicians.blogspot.com kwa kupeleka matangazo, picha za matukio mbalimbali hata ya shughuli binafsi kama birthday, harusi na  kadhalika na pia kutuma hata nyimbo zao ili ziweze kutundikwa katika mtandao huo bure bila malipo. Wanamuziki walielekezwa kutuma kazi zao kupitia anwani ya musicnettz@gmail.com.
Katibu Mkuu wa mtandao Abraham Kapinga, alitoa maelezo kuhusu hali ya ofisi, ambapo wanamuziki walielezwa kuwa ofisi iko Kinondoni karibu na American Chips, mtaa wa CHADEMA, na kwa vile ndio tumekabidhiwa ofisi, wanamuziki waliafikiana kukutana hapo na kuifanyia ofisi usafi, jambo ambalo nalo lilionyesha nia ya wanamuziki kulea chama chao. Mwanamuziki Hussein Jumbe alijitolea viti 4 kwa ajili ya ofisi, jambo ambalo kwa kila hali ni la kutia moyo kuhusu mwanzo huu wa mtandao.
Mweka hazina wa Mtandao Asha Salvador alitoa taarifa ya vifaa vya ofisi vilivyonunuliwa vikiwemo viti, meza feni, na stationary.
Maelezo mengine muhimu yaliyotolewa ni kuhusu wanamuziki kujiunga na chama, na kulipia ada ili kuweza kuendesha ofisi. Fomu za wanachama ni shilingi 1000/- ada ya mwaka 5,000/- na kiingilio ni shilingi 20,000/-.
Wajumbe walipata muda wa kutoa mawazo na mapendekezo. Mjumbe mmoja alitoa mapendekezo ya mtandao kuwezesha wanamuziki kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya  Katiba ya nchi na  mjumbe mmoja alijitolea kufuatilia taratibu za kuhakikisha wanamuziki wanashiriki katika jambo hilo muhimu.  Mjumbe mwingine alitaka Mtandao uandae program za elimu ya Management ya Band na hata elimu kwa wanamuziki kujitambua na hivyo sio kufika mahala kuporomoka baada ya muda mfupi, pia itolewe elimu kuhusu haki mbalimbali za wanamuziki. Mmoja wa wajumbe alieleza kuwa ametoka nje ya nchi karibuni alikopata elimu ya vocal training, na hivyo Mtandao uandae taratibu ili elimu hii iwafikie wanamuziki waimbaji.
Mjumbe mmoja alitoa taadhari kuhusu hali inayoelekea sasa ambayo inafanya kuweko na uhasama kati ya wanamuziki wa kizazi kipya na wale wa zamani, badala ya wote kutambuana kuwa ni wanamuziki wanaoweza kufanya kazi pamoja na kupata mafanikio makubwa zaidi, Mtandao uliombwa uwe chombo cha kuunganisha wanamuziki wote bila kujali aina ya muziki wa rika.
Swala la vyombo vya utangazaji liliongelewa hasa kuhusu rushwa iliyokithiri katika vyombo hivi ikawekwa hadharani. Mjumbe mmoja alieleza kuwa imefikia kuwa inahitajika shilingi milioni moja kuwezesha wimbo kupigwa katika radio, kwani kuna mgao wa kuanzia mtu anaweka nyimbo kwenye playlist hadi watangazaji wa vipindi mbalimbali kwa ajili ya kupiga muziki na interviews. Ilionekana tatizo hilo lipo hata kwenye radio zinazopiga muziki wa Gospel ambako tofauti ni bei tu. Ambapo bei ya kupigwa wimbo ni kati ya shilingi alfu 80 hadi laki moja. Mtandao ulitakiwa ufuatilie utekelezaji wa sheria ya kulipia matumizi ya muziki katika vyombo vya utangazaji, ambayo ilikuwa ianze kutumika toka 2003.
Wanamuziki walimaliza siku kwa kutumia muda kujaza fomu za uanachama.






Sunday, August 11, 2013

MKUTANO WA WANAMUZIKI JUMANNE 13 AGOSTI 2013 BASATA

MTANDAO wa Wanamuziki utakuwa na  mkutano  wa wanamuziki siku ya Jumanne tarehe 13 kuanzia saa 4 hadi saa 6 pale BASATA Ilala Sharif Shamba.kati ya mambo yatakayofanyika ni kuhamasisha uandikishaji wa wanachama wapya, na pili kupata taarifa ya mpango wa Bima ya Afya kwa wanamuziki. Wanamuziki wote na wadau wengine wanaofanya kazi katika tasnia hii ya muziki, wakiwemo pia waalimu wa muziki, producers, wacheza shoo, mameneja na kadhalika

Monday, August 5, 2013

UJUE MTANDAO WA WANAMUZIKI TANZANIA, hali halisi sasa na malengo kwa muda mfupi ujao

TANZANIA MUSICIANS NETWORK ni mkusanyiko ya wadau wote wanaofanya kazi kwa njia moja au nyingine katika tasnia ya muziki. Muziki hapa ukiwa na maana ya mapana yake yote, muziki wa vikundi na ule wa watu mmoja mmoja, na bila kuwa na mipaka ya aina ya muziki na bila kujali kama ni muziki asili au muziki mapokeo, hivyo kila mtu anaefanya kazi ya muziki bila kujali umaarufu wake au aina ya muziki wake anakaribishwa. Chama pia kinakaribishwa watendaji wengine katika muziki kama vile mameneja , maproducer wa audio na video, mafundi mitambo wa studio na wale wa 'live', dancers maarufu kama stageshow, na wachezaji wa ngoma za asili. 
Wanachama wa Mtandao ni watu binafsi na si vikundi.
Mtandao una lengo la kuwakusanya wadau katika tasnia hii kuwa na sauti moja ili kuweza kurekibisha taratibu za utendaji katika tasnia hii na kuwawezesha wahusika wote kupata stahili zao kama inavyotakiwa. Mtandao ni mwanachama hai wa International Federation of Musician na hivyo moja ya malengo ya Shirikisho hilo ni kuhakikisha kazi ya muziki inatambuliwa kama ajira nyingine na hivyo kutungiwa sheria za kazi na taratibu za kazi kama kazi nyingine, na hivyo mtandao nao kulenga kufikisha hali hiyo kwa wanamuziki wa Tanzania. Kwa kipindi hiki cha awali ajenda nyingine kubwa ni kuweza kufanikisha kupatikana kwa Bima za Afya kwa wanamuziki wanachama mazungumzo yamekwisha anza na vyombo husika ili hili liwe limeanza kutekelezwa kabla ya mwisho wa mwaka.
Kwa wakati huu Mtandao uko chini ya uongozi wa muda 
Mwenyekiti:  John Kitime -Mwanamuziki Kilimanjaro Band
Katibu Mkuu: Abraham kapinga- Mwanamuziki Tanzanite band
Mweka Hazina: Asha Salvador- mwanamuziki Hisia Sound
Mpaka sasa kuna kamati mbili, zenye wanamuziki mchakanyiko vijana na wakongwe, ambazo ziko kazini
i. kamati ya utawala ambayo imewezesha kupatikana kwa ofisi na baadhi ya vifaa vyake na sasa inaanza taratibu za uandikishaji wa wanachama
ii. kamati ya fedha ambayo inaratibu mapato na matumizi ya fedha.
Kamati ya tatu itaanza kazi kabla ya tarehe 15 mwezi huu ambayo itashughulikia na utayarishaji wa ripoti ya hali halisi ya shughuli za Hakimiliki, jambo ambalo litahusisha researchers wa ndani na nje ya nchi, workshop kubwa ya wanamuziki mwezi wa tisa, na hatimae shughuli nzima kutoa ripoti ambayo itaweza kutumika na vyombo mbalimbali vinavyohusika na muziki na ripoti itasaidia sana Serikali kuanza kutoa maamuzi sahihi.

Sunday, August 4, 2013

MASHUJAA BAND YATAMBULISHA NYIMBO ZAKE ITAKAZO REKODI


Jana Jumamosi  tarehe 3 Agosti, bendi ya Mashujaa ilifanya jambo ambalo ni nadra kufanyika katika bendi siku hizi. Bendi hii ilialika wadau na wapenzi wa bendi ili waweze kuzisikiliza nyimbo ambazo bendi hii inatarajia kuzirekodi. Bendi ilipiga mfululizo wa nyimbo  tano, zilizokuwa katika miondoko mbalimbali . Kwa ujumla bendi ina waimbaji wazuri sana kadri ya mazingira ya uimbaji wa siku hizi. Nyimbo zilikuwa nzuri japo zingeweza kuwa bora zaidi kwa kuongeza effects katika magitaa, na urekibishaji wa sauti  kwa ujumla(maarufu kama setting) , japo ungeboreshwa zaidi. Tatizo la setting ya vyombo kwa ujumla limekuwa sugu kwa bendi nyingi, kiasi kuwa kama ni kawaida kukuta sauti zikitoka kwa kikwaruzo na mara nyingine kutosikia waimbaji wanatamka nini katika wimbo.
Album hii itakuwa na mvuto kwa wapenzi wa muziki wa sebene, na pia ni album ya kwanza baada ya bendi hii kubeba tuzo tano katika Kili Music Awards karibuni.
Kati ya wadau waliokuweko katika shughuli hii ni wakali kama deo mwanatanga, William kaijage, Mafumu Bilali, Khalid Chokoraa, Khamis Dacota, John Kitime na wengine wengi walitoa mawazo yao kila baada ya wimbo kwisha ni jambo zuri kama litaendelezwa na pia kama litachukuliwa kwa uzito unaostahili na wanamuziki kwa upande wao.






Saturday, August 3, 2013

TAAARIFA YA MSIBA--AGE KAUZENI HATUNAE TENA

Mwanamuziki wa zamani wa Biashara Jazz Band na JUWATA Jazz Band Agae Kauzeni hatunae tena. Kwa maelezo ya Mwanamuziki Bonzo Kwembe, marehemu amekuwa anaugua kwa kipindi cha mwezi mmoja.Agai amefariki leo Visiga Kibaha. Na mipango ya mazishi inafanyika ili mazishi yawe kesho Kibaha Mnemera. Mungu Amlaze pema peponi