Tuesday, September 29, 2015

MWANAMUZIKI WA DOUBLE M SOUND AVAMIWA NA VIBAKA MSUMBIJI


Taarifa zimetufikia kwenye ofisi ya Mtandao wa Wanamuziki Tanzania, kutoka kwa Muumin Mwinjuma 'Kocha' zikieleza kuwa mmoja wanamuziki wake aliokuwa nao katika safari ya Msumbiji amepata mkasa wa kuibiwa na kuumizwa muda mfupi kabla ya onyesho kumalizika rasmi. Kwa kadri ya maelezo ya Muumini, bendi ilipiga katika kitongoji cha Nanyupu, ambapo show hiyo ilikuwa ni ya pili katika mahala hapo baada ya bendi kufanya show ya kwanza siku ya Jumapili tarehe 20 Septemba. Kitongoji hiki ni makazi ya wachimbaji wa madini ya Ruby ambapo wengi wao ni Watanzania, pia kuna wenyeji ambao ni Wamsumbiji, Wasenegali na Wanaijeria kadhaa. Kwa kuwa Watanzania ni wengi, mara baada ya show ya kwanza, wakazi walimuomba aliyeipeleka bendi wakapige show nyingine, nae hakukataa kwani alikuwa katengeneza pesa vizuri, hivyo bendi ilikwenda kupiga tena siku ya Alhamisi tarehe 24 Septemba, siku ya Idd. Wakati wa kupiga wimbo wa mwisho, muimbaji Amina hakuwa na kazi hivyo alishauriana na madansa watangulie kwenye gari. Madansa waliondoka kwa pamoja na kuelekea kwenye gari lakini Amina ambaye pia ni katibu wa bendi alipanda kwanza jukwaani kumuaga Muumini. Aliposhuka kwenye jukwaa kuelekea kwenye gari kundi la vijana wakaanza kumsemesha Kiswahili nae akawa anajisikia kama yuko na ndugu zake. Vijana wale ghafla wakamvamia na kuanza kumpiga makofi na kumburula na kumpora mkoba wake uliokuwa na passport yake na ya mpiga drum na fedha za Msumbiji zenye thamani ya 150,000/-. Wenzie walipofika kumsaidia tayari vibaka wale walikuwa wameshaingia gizani.  Na mara moja dansi lilivunjwa ili kumpeleka mji wa Pemba kwa matibabu.
Bendi ilifanya maonyesho mengine mawili katika mji wa Pemba na kuona kuna haja ya kurudi kwanza nyumbani ili Amina apone vizuri, wakati wanamuziki wengine wanategemea kurudi nchini wakati wowote, Amina ataendelea kuwa Msumbiji kwa wiki moja zaidi ili apate matibabu zaidi. Pia bendi inakuja  kujipanga kwa safari ndefu zaidi inayotegemewa muda si mrefu.
Amina akiwa na mwanamuziki mwenzie Kupaza


Monday, September 21, 2015

DAVID NG'ASI MWANACHAMA WA MTANDAO WA WANAMUZIKI AFIWA NA BABA YAKE

MWANACHAMA WA MTANDAO WA WANAMUZIKI ambaye ni mpiga piano na mwalimu wa piano amefiwa na baba yake mzazi Mzee Aloysi Ng'asi nae alikuwa mwalimu wa muziki aliyeheshika sana katika nyanja hiyo.Mzee Ng'asi aliyezaliwa huko Iringa amezikwa Kinondoni
David akisimika msalaba kwenye kaburi la baba yake

DOUBLE M YAANZA KUTIKISA MSUMBIJI

KUNDI  la Double M chini ya Muumin Mwinyjuma, limealikwa Msumbiji kwa mwezi mzima, na katika wakati huo kundi litashiriki katika sherehe za miaka 51 ya Vita vya Ukombozi wa nchi hiyo. Wanamuziki hawa ambao ni wanachama wa Mtandao wa Wanamuziki walipitisha barua yao ya taarifa ya kwenda huko na hivyo Mtandao ukatoa taarifa Baraza la sanaa La Taifa kama inavyostahili. Waliomo katika msafara huo ni pamoja na kiongozi wa kundi Muumin Mwinyjuma,  maarufu kwa jina la KOCHA, na wanamuziki wengine 16.
1.     Mwinjuma Muumin Buguza- Kiongozi wa Bendi-Muimbaji
2.     Omary Kisila- Kinanda
3.     Hamza S Waninga- Drums
4.     Imma Keffa –Bass Guitar
5.     Emmanuel Namwinga- Rhythm guitar
6.     Amina R Juma –Muimbaji
7.     Veronica D Buzeri –Dansa
8.     Neema Kawambwa-Dansa
9.     Stamili  Hamis –Dansa
10. Greyson Semsekwa – Rapper
11. Sharey Aboubakar-Muimbaji
12. Revina Mzinja -Dansa
13.  Salma Shaaban –Dansa
14. Afande Muhamada-Fundi Mitambo
15. Omary Maulid –Fundi Mitambo
16. Saleh Kupaza-Muimbaji
17. Dogo Rama-Muimbaji











Habari toka TAMUNET- Mtandano wa Wanamuziki Tanzania

Monday, September 14, 2015

MWANAMUZIKI KUIBURUZA KAMAPUNI YA SIMU MAHAKAMANI


MWANAMUZIKI wa Abuja, nchini Nigeria Omenuwoma Okson Dovie, aka Baba 2010, ameamua kuipeleka mahakamani kampuni ya simu ya  MTN kwa kukiuka haki zake za hakimiliki katika nyimbo zake nne, zikiwemo "Gentleman "Ometena", "Twisted" and "Unity Song."
Dovie anaituhumu kampuni hiyo kwa kubadili nyimbo hizo kuwa caller tunes/ring tones, na kuziuza bila ruksa yake kwa miaka mitatu mfululizo. Nyimbo hizo ziko kwenye album yake aliyoitoa 2005 ikiwa na jina
 "Twisted”.
Barua ya mwanasheria wake Rockson Igelige, imeitaka  MTN kumlipa mteja  wake naira milioni 500 (Tshs 5,455,000,000), kwa matumizi ambayo hayakuruhusiwa na yenye kupunguza thamani ya nyimbo zake. Na pia alitoa siku 14 ambazo MTN lazima iwe imekamilisha malipo au kujibu hoja.
Mshauri wa sheria wa MTN amekubali kuwa kapokea barua na kuwa kampuni hiyo inaliangalia swala hilo. Wakati huohuo Igelige amesema wameishauri Kamisheni ya Hakimiliki ya Nigeria kuwafungulia mashtaka MTN, wakati nao wakifungua mashtaka kwa upande wa mwanamuziki.

Wednesday, September 2, 2015

WANAMUZIKI WACHANGAMKIA KUPATA BIMA YA AFYA

Hamis Mnyupe wa Msondo akijaza fomu za Bima ya Afya

Kinuka, mpiga bezi wa kujitegemea na producer akijaza fomu za Bima ya Afya

Goddy Mkude mpiga gitaa wa B Band akijaza fomu za Bima ya Afya




Geophrey Kumburu mpiga kinanda na producer akiwa na kadi yake ya Bima aliyoipata karibuni


Simon Mwamkinga mpiga kinanda na kiongozi  wa Rungwe Band akiwa na kadi yake ya Bima ya Afya aliyoipata karibuni

TAMUNET YAWEZESHA WANAMUZIKI KUPATA BIMA YA AFYA


Mwaka 2004, John Kitime ambaye kwa sasa ndie Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (Tanzania Musicians Network-TAMUNET) alihudhuria Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Muziki Duniani –International Federation of Musician (FIM). Katika mkutano huo moja ya maazimio ya mkutano ule ilikuwa kila nchi ihakikishe inaanzisha utaratibu wa Bima ya Afya kwa wanamuziki wake. 
Mara baada ya kurudi Tanzania, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa TAMUNET, Kitime alianza kufuatilia uwezekano wa kupata huduma ya Bima hiyo kwa wanamuziki. Kwa bahati mbaya hakukuwa na njia yenye gharama nafuu ya malipo ya BIma hiyo ambayo mwanamuziki wa kawaida angeweza kuyamudu. Kulikuweko na kampuni ambayo iliweza kutoa huduma hiyo kwa gharama ya dola 300 kwa mwaka kwa mwanamuziki mmoja. Kampuni nyingine za Bima zilizotembelewa hazikuonyesha ushirikiano katika jambo hilo. TAMUNET iliwasiliana pia na mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa katika kipindi hico mfuko ulikuwa hauna mamlaka ya kuhudumia watu waliokuwa nje ya ajira ya serikali na mashirika ya umma. TAMUNET iliwasiliana na Mganga Mkuu wa Serikali, ambaye alishauri TAMUNET kuwasiliana na NGO moja ambayo ilikuwa na makao yake makuu Sinza, na kweli NGO hiyo ilikubali kuwa ingeweza kutoa huduma ya Bima ya Afya kwa wanamuziki kwa gharama ya shilingi 3000/- tu kwa mwezi, lakini huduma hii ilikuwa ni kwa hospitali kadhaa tu jijini Dar es Salaam. Hilo nalo lilionekana ni bora kuliko kukosa kabisa, lakini muda mfupi baadae NGO hiyo ilisema haishughuliki tena na huduma hiyo bali imeelekeza nguvu zake kwa watoto wa mtaani. Hapo ilifuatia miaka kadhaa ambayo hakukuweko na njia yoyote iliyowezekana ya kupata huduma hiyo. TAMUNET ilijaribu pia kuwasiliana na mifuko mingine, lakini kila mara iligonga ukuta aidha kwa ahadi ambazo zilikuwa zikipigwa kalenda bila kutekelezwa.
Mwaka 2015 hatimae ndipo mlango umefunguka, Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa NHIF, uliitarifu TAMUNET kuwa umeanzishwa mpango wa Bima kwa Kikoa ambao ungewawezesha wanamuziki nao kupata Bima ya Afya kwa gharama nafuu. TAMUNET iliuchangamkia mpango huo kwa kuwa imekuwa ajenda ya chama hiki kwa miaka zaidi ya kumi.
Wanamuziki wanachama wa TAMUNET tayari wameanza kufaidi huduma ya Bima ya Afya kwa mwaka mzima, hii ni baada ya kulipia shilingi 76,800/-. Mpango huu utaondoa aibu ya wanamuziki kuchangiwa fedha za matibabu kila wanapougua, kwani itakuwa busara kwa wapenzi na washabiki wa muziki kuchangia mwanamuziki wanaempenda apatiwe Bima ya Afya kuliko kumchangia fedha za matibabu ya muda mfupi. Baadhi ya wanamuziki ambao tayari wana bima za afya chini ya mpango huu ni Louiza Nyoni, Abdul Salvador, Rashid pembe, na wengine wengi wamekwisha anza taratibu za kupata huduma hii.
Wasanii katika semina kuhusu BIma Ya Afya iliyofanyika BASATA karibuni

Muwezeshaji Catherine kutoka Mfuko wa Taifa wa BIma ya Afya akitoa maada katika semina ya wasanii kuhusu Bima ya Afya

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Paul Makond aliyekuwa mgeni rasmi katika semina ya Bima ya Afya kwa wasanii

Mwenyekiti wa TAMUNET akipokea kadi za kwanza za Bima ya Afya za wanamuziki, katika ofisi za Mfuko wa BIma ya Afya wa Taifa.

John Kitime akiwa na kadi yake ya BIma ya Afya aliyoipata karibuni

Kadi za Bima ya Afya za wanamuziki mbalimbali



Louiza Nyoni akionyesha kadi yake mpya ya Bima ya Afya
Ushirikiano wa Mfuko wa Biam ya Afya na TAMUNET unaweka uwezekano wa mwanamuziki kuanza kuchanga hata fedha kidogokidogo ili kuweza kufikisha kiasi kinachotakiwa. Wanamuziki wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe kwenue simu na 0763722557 ili kupata maelezo ya namna ya kujiunga na huduma hii. Ukiwa mwanamuziki wa Hiphop, taarab, muziki asili, dansi bongofleva, huduma hii ni kwa ajili yako kumbuka WAJANJA HUJIWEKEA BIMA YA AFYA- NA WEWE NI MMOJA WA WAJANJA

Thursday, May 21, 2015

VANESSA MDEE AFIWA NA DADAKE MKUBWA

Muimbaji mahiri Vanessa Mdee amefiwa na dada yake mkubwa Anna Mdee, ambaye amefariki katika hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam,  jana Jumatano alfajiri. Anna ambaye alikuwa mfanya kazi wa kampuni ya sigara ya TCC na alikuwa katika kituo cha Dodoma kwa muda mrefu alikuwa India akipatiwa matibabu.
Anna na Vanessa ni watoto wa marehemu Sammy Mdee, aliyekuwa mwandishi mkongwe aliyewahi kuongoza gazeti la Daily News, Katibu wa Mwalimu Nyerere na pia mkurugenzi wa kituo cha AICC. Mazishi ya Anna yatakuwa Same Jumamosi mchan saa 8.
Mungu Amlaze Pema Anna Mdee

Wednesday, April 29, 2015

MTANDAO WA WANAMUZIKI WAWEZESHA WANAMUZIKI KUPATA HUDUMA YA BIMA YA AFYA

Wanamuziki wanachama wa Tanzania Musicians Network -TAMUNET_ sasa wanaweza kujiunga na mpango nafuu wa Bima ya Afya baada ya chama chao kuingia katika makubaliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF.
WAnamuziki walikuwa ni kundi mojawapo ambalo limekuwa na tatizo kubwa la kupata matibabu bora kutokana na kukosa taratibu za bima ya afya, jambo ambalo ni njia ya kisasa na ya uhakika wa kupata matibabu bora kwa kila binadamu.
Katika kikao cha viongozi wa chama hicho leo kamati maalumu imeundwa kuratibu mpango huu ambapo kamati hii itakuwa ikiandikisha wanachama wote wanaohitaji kupata huduma hii muhimu. Kamati itakuwepo kila Jumatano kuanzaia saa nne mpaka saa tisa katika ofisi za Mtandao zilizopo katika jengo la ghorofa lililojengwa kwa matofari ya kuchomwa jirani na hospitali ya Mvungi katika barabara ya kuelekea mahakama ya Kinondoni, chumba namba 148. Pia unaweza kuwasiliana na Mweka hazina Asha Salvador kupitia simu namba 0687378797 kwa maelezo ya ziada