Tuesday, September 29, 2015

MWANAMUZIKI WA DOUBLE M SOUND AVAMIWA NA VIBAKA MSUMBIJI


Taarifa zimetufikia kwenye ofisi ya Mtandao wa Wanamuziki Tanzania, kutoka kwa Muumin Mwinjuma 'Kocha' zikieleza kuwa mmoja wanamuziki wake aliokuwa nao katika safari ya Msumbiji amepata mkasa wa kuibiwa na kuumizwa muda mfupi kabla ya onyesho kumalizika rasmi. Kwa kadri ya maelezo ya Muumini, bendi ilipiga katika kitongoji cha Nanyupu, ambapo show hiyo ilikuwa ni ya pili katika mahala hapo baada ya bendi kufanya show ya kwanza siku ya Jumapili tarehe 20 Septemba. Kitongoji hiki ni makazi ya wachimbaji wa madini ya Ruby ambapo wengi wao ni Watanzania, pia kuna wenyeji ambao ni Wamsumbiji, Wasenegali na Wanaijeria kadhaa. Kwa kuwa Watanzania ni wengi, mara baada ya show ya kwanza, wakazi walimuomba aliyeipeleka bendi wakapige show nyingine, nae hakukataa kwani alikuwa katengeneza pesa vizuri, hivyo bendi ilikwenda kupiga tena siku ya Alhamisi tarehe 24 Septemba, siku ya Idd. Wakati wa kupiga wimbo wa mwisho, muimbaji Amina hakuwa na kazi hivyo alishauriana na madansa watangulie kwenye gari. Madansa waliondoka kwa pamoja na kuelekea kwenye gari lakini Amina ambaye pia ni katibu wa bendi alipanda kwanza jukwaani kumuaga Muumini. Aliposhuka kwenye jukwaa kuelekea kwenye gari kundi la vijana wakaanza kumsemesha Kiswahili nae akawa anajisikia kama yuko na ndugu zake. Vijana wale ghafla wakamvamia na kuanza kumpiga makofi na kumburula na kumpora mkoba wake uliokuwa na passport yake na ya mpiga drum na fedha za Msumbiji zenye thamani ya 150,000/-. Wenzie walipofika kumsaidia tayari vibaka wale walikuwa wameshaingia gizani.  Na mara moja dansi lilivunjwa ili kumpeleka mji wa Pemba kwa matibabu.
Bendi ilifanya maonyesho mengine mawili katika mji wa Pemba na kuona kuna haja ya kurudi kwanza nyumbani ili Amina apone vizuri, wakati wanamuziki wengine wanategemea kurudi nchini wakati wowote, Amina ataendelea kuwa Msumbiji kwa wiki moja zaidi ili apate matibabu zaidi. Pia bendi inakuja  kujipanga kwa safari ndefu zaidi inayotegemewa muda si mrefu.
Amina akiwa na mwanamuziki mwenzie Kupaza


No comments:

Post a Comment