Monday, November 23, 2015

JE WEWE NI MSANII WA BONGOFLEVA? USIKOSE HII


JOHN KITIME ATOA ELIMU YA HAKIMILIKI KWA VIONGOZI WA VYAMA NA VIKUNDI VYA SANAA

MWENYEKITI  wa Mtandao wa Wanamuziki Tanzania, John Kitime, siku ya tarehe 19 Novemba 2015, alitoa semina ya Hakimiliki kwa zaidi ya wasanii 50 waliokuwa katika warsha iliyoandaliwa na Baraza la Sanaa La Taifa (BASATA). Katika semina hiyo iliyotambulika kama Capacity Buildingfor Art Association and Group Leaders in Tanzania ilifanyika Ilala Shariff Shamba zilipo ofisi za BASATA. Kitime aliweza kuwafahamisha washiriki nini maana ya Hakimiliki, matumizi yake mipaka yake na kugusia sheria ya Hakimiliki ya Tanzania inavyofanya kazi. John Kitime ambaye amekwisha fanya semina za aina hii katika nchi mbalimbali Afrika zikiwemo Ghana, Malawi, Senegal amekwisha karibishwa Kenya kufanya semina za aina hiyo.

WASHIRIKI MBALIMBALI WAKIKABIDHIWA VYETU VYA USHIRIKI


STELLAH JOEL





RAY

BRAITON


KAKA GANO





Tuesday, November 17, 2015

TAMASHA LA KUMSHUKURU MUNGU SASA KUFANYIKA DESEMBA 25 DIAMOND JUBILEE

 Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akifafanua jambo kwa umakini mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki kuhusu maandalizi ya tamasha la kumshukuru Mungu kwa amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu litakalofanyika Desemba 25.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki kuhusu maandalizi ya tamasha la kumshukuru Mungu kwa amani na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu litakalofanyika Desemba 25.

KAMPUNI ya Msama Promotions imeamua kuandaa Tamasha la muziki wa Injili litakalofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumshukuru Mungu nchi kuvuka salama katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, alisema wameamua kuua ndege wawili kwa jiwe moja, kwani sasa litafanyika Desemba 25, likibeba Sikukuu ya Krismasi na shukrani hiyo ya kuvuka salama katika Uchaguzi Mkuu.

Alisema kutokana na tamasha hilo kubeba ajenda hizo mbili kwa pamoja, kamati yake imelipa uzito mkubwa kwa upande wa suala la  maandalizi ambapo wameanza kuzungumza na waimbaji nguli wa kitaifa na kimataifa.

Msama alisema baada ya tamasha hilo kufanyika Desemba 25 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, litahamia katika mikoa mbalimbali itakayoteuliwa na kamati yake kwa kuzingatia kigezo cha wingi wa maombi na uwezo wao kifedha.

“Naomba ifahamike, tamasha hili la kumshukuru Mungu kuiwezesha nchi kuvuka salama katika mtihani mgumu wa Uchaguzi Mkuu uliokuwa na ushindani mkubwa, litafanyika Desemba 25 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee,” alisema Msama na kuongeza:

“Unaweza kuona ni tamasha ambalo safari hii litakuwa na uzito mkubwa, kwani litakuwa limebeba uzito wa Krismasi itakayoambatana na shukrani maalumu kwa Mungu kutokana na kuijalia nchi kuvuka salama katika Uchaguzi Mkuu,” alisisitiza Msama.

Kuhusu waimbaji, Msama alisema kamati yake itajitahidi kuwaleta wenye uzito na mvuto kulingana  na uzito wa tamasha hilo, akiamini litakuwa na mvuto wa tofauti na yaliyotangulia na kuwasihi wapenzi na mashabiki wa muziki wa Injili kukakaa mkao wa kupokea baraka za Mungu.

Msama kupitia Kampuni yake ya Msama Promotions, amechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa Injili nchini kupitia ubunifu wake wa kuratibu matukio ya muziki huo kuanzia tamasha la Pasaka, Krismasi na uzinduzi wa kazi za waimbaji mbalimbali.

Juhudi hizo za Msama ndizo zimeufanya muziki wa Injili kupata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kiasi cha kuwa moja ya ajira kwa vijana wenye vipaji na karama ya kumtumikia Mungu kwa njia hiyo ya uimbaji.

Thursday, November 12, 2015

KATIBU MKUU WA WIZARA YA HABARI VIJANA UTAMADUNI NA MICHEZO ATEMBELEA BASATA


IMG_20151112_131420 Prof Elisante akiongea na akina mama wanaofanya sanaa ya kutengeneza Batik katika maeneo ya BASATAIMG_20151112_211008 Toka kushoto Godfrey Mngereza, Katibu Mtendaji BASATA, Prof Elisante Ole Gabriel, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, John Kitime Mjumbe wa Bodi BASATA, Kaimu Mkurugenzi wa Utamaduni 
KATIBU mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni na Vijana na Michezo Prof Elisante Ole Gabrielleo ametembelea Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Katibu MKuu baada ya kuzunguka na kuangalia maeneo yote ya Baraza, hatimae alikuwa na mkutano na wafanya kazi wa Baraza. Katika mkutano huo Katibu Mkuu alisema ametembelea Baraza ili kufahamiana,na pia kufafanua kauli mbiu ya Rais ya HAPA KAZI TU.
Katibu Mkuu alisifia Baraza kwa kusimamia sheria na taratibu zilizounda Baraza hilo. Profesa alilitaka Baraza kuhakikisha kuwa linakuwa na ufanisi zaidi na pia kuwezesha kutafuta masoko ya uhakika ya kazi za sanaa. Tanzania ina kazi nyingi sana za sanaa hivyo alilitaka Baraza kuhakikisha zinafahamika zinatangazwa, na zinasambazwa, ili kuleta manufaa kwa wasanii na kuchangia pato la nchi kwa kodi. Katibu Mkuu aliagiza kuwa viongozi wa Baraza wawe mfano katika utendaji wa kazi, heshima kwa watumishi wote na pia wawe waadilifu katika kazi zao. Katibu Mkuu aliwaasa watumishi wa Baraza kuipenda kazi yao kuwa wazalendo na kuwajibika ipasavyo, kuheshimu viongozi na kuwasiliana kwa staha pale kunapokuwa na tatizo. Aliwakumbusha wafanya kazi kuwahi kazini lakini pia alikumbusha uongozi kutokuwaweka wafanya kazi masaa ya ziada bila ya sababu za msingi, kwani wanahtaji kupumzika baada ya kazi za siku nzima. Aliwaonya watumishi kuhusu ‘majungu’ na kuwataka waepuka jambo hilo kwani ni chanzo cha kuharibu kazi. Kabla ya hotuba hii Katibu Mtendaji alimueleza Katibu Mkuu kuhusu changamoto za Baraza na baadhi ya njia ambazo zingefanywa kutatua changamoto hizo. Katibu Mkuu alisema kuwa yeye haridhiki na hali ya uchumi ya wasanii na alitaka Baraza lifanye kazi kubadili hali hii. Na mwisho alisisitika kuwa kauli ya Hapa Kazi tu ni ya ukweli na kila mtu aishi kwa kauli mbiu hiyo.
Kabla ya maelezo haya Katibu Mtendaji wa Basata alitoa baadhi ya changamoto za uendeshaji wa BASATA. Kati ya changamoto hizo alizitaja kuwa ni ukosefu wa sera za sanaa, kupitwa na wakati kwa sheria iliyounda Baraza. Mtawanyiko wa asasi zinazotawala wasanii. Ukosefu wa masoko ya sanaa, kutokukamilika kwa ukumbi wa BASATA, tatizo la siasa kujikita katika sanaa, na pia uhamasishaji wa Bima ya Afya kwa wasanii.
Katibu Mtendaji alimkabidhi Katibu Mkuu, nyaraka zote zilizotayarishwa kuhusu changamoto hizo

Thursday, October 29, 2015

KATIBU MTENDAJI WA BASATA AMKABIDHI MZEE MAPILI KADI YAKE YA BIMA YA AFYA

Katibu Mtendaji wa BASATA Bwana Ngereza, Mzee Mapili na Mama Shalua mmoja wa maafisa wa BASATA
KUPITIA mpango unaoratibiwa na TAMUNET, ambapo Mtandao huu umeingia makubaliano na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa HHIF, mwanamuziki mkongwe wa siku ntingi ameweza leo kukabidhiwa kadi ya Bima ya Afya. Akikabidhiwa kadi hiyo Mzee Mapili alishukuru Mtandao wa Wanamuziki, na kusema kuwa mpango huu utamsaidia sana kwani ana matatizo ya moyo na figo na anahitaji matibabu na dawa za mara kwa mara. Katibu Mtendaji wa BASATA aliwashauri wanamuziki na wasanii wengine kujiunga na Bima ya Afya

Monday, October 26, 2015

DIAMOND ATWAA TUZO YA MTVEMA


HAKIKA Diamond kiboko yao. TAMUNET inatoa hongera kwa  Diamond Platnumz kwa kushinda MTV European Music Awards (MTVEMA), katika tukio lililofanyika Milan  Jumapili hii tarehe  25 October wakati Tanzania ikipiga kura kutafuta viongozi wake wa miaka mitano ijayo. Tuzo hili hufanyika katika miji mbalimbali ya Ulaya kila mwaka, na washindi huchaguliwa kwa kura za wapenzi kutoka dunia nzima. Mcheza filamu kutoka India na ambae pia alikuwa Miss  World mwaka 2000 Priyanka Chopra pia alishiriki akiwa kundi moja na Diamond, katika ‘ category ‘ ya  Worldwide Act : "Africa/ India". Pamoja na uwingi wa watu wa India , Diamond Platnumz ameweza kupata kura nyingi zaidi na kuongeza sifa wake mwenyewe binafsi na kwa Taifa. Hongera tena Diamond
Priyanka Chopra

Saturday, October 24, 2015

Profesa Elisante Ole Gabriel ateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa Ijumaa, Oktoba 23, 2015, amewateua Makatibu Wakuu wanne wapya wa wizara mbali mbali. Kati Makatibu Wakuu hao Rais amemteua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel, kuwa Katibu Mkuu na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Sihaba Nkinga kuhamishiwa Wizara ya Wanawake, Jinsia na Watoto kutoka Wizara ya Habari. Hakika hii ni habari nzuri kwa wasanii katika kipindi hiki tunapongojea matokeo ya uchaguzi Mkuu. Profesa ni mchapa kazi wa ukweli, ni kati ya mambo mazuri makubwa yaliyotokea katika Wizara hii kwa muda mrefu

Wednesday, October 21, 2015

DOUBLE M WAKO MSUMBIJI KWA MARA YA PILI



Baada ya kazi nzuri ya awali Double M Sound chini ya Muumin Mwinyjuma imealikwa tena Msumbiji. Kwa maneno yake mwenyewe kiongozi huyu wa kundi hilo alituma ujumbe huu, “Nipo  njiani na vijana wangu tunaenda Msumbiji, tumepata mualiko  mwingine, safari hii tumealikwa na serikali kupitia Manispaa ya Mkoa Wa PEMBA, baada ya kufurahishwa na kazi yetu ya mwezi uliopita. Kuna sherehe ya Kitaifa ambayo hua inazunguka kila Mkoa na mwezi huu inafanyika ktk Mkoa Wa Mpemba, kutakua na burudani za aina nyingi  tofauti. Safari Hii tumetakiwa kuwa na idadi ya watu 14 tofauti na safari ya kwanza tulikwenda 19.
Kwenye msafara wetu tupo watu 13 na mwenzetu mmoja fundi mitambo na mpiga tumba Omar Zagalo alibaki kule na vyombo toka tulipoenda mara ya kwanza. Tulio kwenye msafara huu ni mimi Muumin Mwinyjuma, Rashid Sumuni-solo, Pascal Kinuka-bass, Issa Ramadhani-kinanda, H Waninga-drums, Amina Juma, Salehe Kupaza na  Dogo Rama waimbaji, madansa ni Verosa,Regina, Salma, Titi na Star. Tunasafiri kwa njia ya bus tukishavuka Boda saa 10 Jioni tutachukuliwa na gari lililoandaliwa na wenyeji wetu, ambayo itatumia saa 1-30 kutufikisha mji wa Msimbwe na hapo tutapanda ndege maalum itakayotupeleka Pemba. Tuombeeni Mungu tufanye vizuri zaidi kwani Show hii ni muhimu sana kujitangaza na kuutangaza muziki wa Bendi za TZ."

Tuesday, October 20, 2015

MSONDO NGOMA WAKUBALIANA KUPATA BIMA YA AFYA.

KATIKA  mkutano uliofanyika leo kwenye makao makuu ya MSONDO, wanamuziki waliweza kupata taarifa ya namna BIMA YA AFYA inavyofanya kazi. Maelezo hayo yaliyotolewa kwao na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanamuziki, (TAMUNET) John Kitime. Baada ya mkutano huo wanamuziki hao walikubaliana kuanza kuhakikisha kila mmoja wao ana Bima ya Afya mara moja