Friday, August 29, 2014

MTANDAO WA MUZIKI WASHIRIKI SAFARI YA KUTEMBELEA BUNGE LA KATIBA DODOMA




Hii ndio PRESS RELEASE  iliyosomwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanamuziki siku ya  27 August 2014 kwa waandishi wa habari jijini Dodoma. Ndugu waandishi wa habari, katika mfumo wa sanaa wa nchi yetu wasanii wamegawanyika katika makundi makuu manne, ambayo yanaendeshwa na Mashirikisho ya vyama mbalimbali vya sanaa. Mashirikisho hayo ni;
i.                Shirikisho la Filamu TAFF
ii.              Shirikisho la Sanaa za Maonyesho
iii.             Shirikisho la Sanaa za Ufundi
iv.             Shirikisho la Muziki
 Tuliopo mbele yenu ni viongozi na wasanii kutoka vyama na Mashirikisho ya sanaa yaliyotajwa hapo juu. Kundi hili limekuwepo hapa Dodoma kwa siku mbili kukutana na wajumbe wa Bunge la katiba ili kufuatilia maslahi ya wasanii katika katika mchakato wa  Katiba mpya ya nchi yetu Tanzania.  Hii si mara ya kwanza kwa kundi hili kukutana na Wabunge wa Bunge hili la Katiba, bali hii ni mara ya tatu kundi hili limefika hapa Dodoma. Mchakato uliotufikisha leo hapa ulianza kwa Mashirikisho kukutana na kutengeneza Baraza la katiba ambapo mashirikisho yalitoa mapendekezo kadhaa yaliyofikishwa kwenye Tume ya Katiba. Lakini hakukuweko jambo lolote lililotokana na mawazo hayo ambalo lilichukuliwa na kuingizwa kwenye Rasimu ya Katiba. Mashirikisho yalituma majina 36, (tisa kutoka kila shirikisho)  katika kupendekeza wawakilishi katika Bunge la Katiba. Katika hili mjumbe mmoja, Paulynus Raymond Mtenda aliteuliwa na hivyo kubeba uwakilish wa kundi zima la wasanii Tanzania. Siku ya Ijumaa 14/2/2014 Mashirikisho yote ya sanaa yalikutana BASATA na kumkabidhi rasmi mapendekezo yao Mbunge huyu, ili ahakikishe kundi hili haliachwi katika mchakato wa Katiba.
Muda mfupi baada ya hapo kundi hili lilikuja Dodoma, na kukutana na Wabunge mbalimbali wa Bunge hili la Katiba, tulikutana na Wabunge wa kambi zote na kufanya nao mikutano mingi, ambayo mingine ilifika mpaka saa nane za usiku. Wabunge wa kambi zote walionekana kuunga mkono hoja za wasanii na tulianza mawasiliano mbalimbali na Wabunge yakiwemo ya ana kwa ana, simu na email, Wabunge wakihitaji documentation mbalimbali kuhusiana na mapendekezo yetu katika Katiba mpya.  Katika kipindi hiki tulikuja wakati hata Mwenyekiti wa Bunde la Katiba hajachaguliwa. Ujumbe huu ulikuja tena …. Na hii ni mara ya tatu.
Ujumbe huu toka awali ulikuwa na maombi mawili tu.
i.                Wasanii kutambuliwa kama kundi maalumu kama yalivyotambuliwa makundi ya wakulima wafugaji, wavuvi. Sababu za kutaka kutambuliwa huku, ni kuwa kundi hili ni kubwa kuliko hata makundi mengine yaliyotajwa hapo juu. Takwimu za Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2006 zinaonyesha kuwa wasanii nchini walikuwa kiasi cha milioni 6. Leo ni mika minane imepita na si siri kuwa kundi hili limekuwa na hivyo kukaribia robo ya Watanzania, si haki kutolitambua.
ii.              Milikibunifu (Intellectual Property) itajwa rasmi kama moja ya aina za mali zinazohitaji kulindwa katika katika Katiba
Tumekuja pia na mapendekezo ya namna ya kuingiza hoja zetu hizi zilizosahauliwa, hatujaja na  Ibara mpya kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoonekana kutuhumu katika magazeti ya juzi. Mapendekezo yetu ni kuwa katika Ibara ya 30 iongezwe  aya moja tu ya. Na ibara ya 37 inayoongelea Haki ya ulinzi wa mali, itambue kuwa pamoja na mali zinazohamishika na zisizohamishika, pia kuna mali isiyoshikika.
Tumepata faraja kubwa kupokelewa na Bunge hili,  Na kuweza kuzunguka kwenye kamati 9 kwa hizi siku mbili kukumbusha mapendekezo yetu haya, ambayo hayabebi tu wasanii bali pia wavumbuzi wa kiteknolojia, kibailojia, wasomi watafiti, na wananchi wote kwa ujumla. Pendekezo letu la pili ni muhimu katika kulinda na kuendeleza uchumi wa Tanzania. Na sisi kama Watanzania tumeona ni muhimu kutumia nafasi hii adimu kuhakikisha tunatoa mawazo yetu katika Bunge hili kwani tusipotumia nafasi hii tutakuwa hatukujitendea haki wala kuvitendea haki vizazi vijavyo vya Tanzania.


SIMON MWAKIFWAMBA-SHIRIKISHOLA FILAMU TANZANIA (TAFF)


JOHN KITIME….MTANDAO WA WANAMUZIKI TANZANIA (TAMUNET)

No comments:

Post a Comment