Ule mkutano ulioitishwa na Tanzania Musicians network (TMN) au Mtandao wa Wanamuziki Tanzania umekuwa wa mafanikio makubwa. Kwanza kwa mahudhurio ya wasanii mbalimbali wakiwemo wanamuziki wa muziki asili, taarab, dansi, bongoflava na gospel, pia kulikuweko na mameneja wa wanamuziki na mabendi mbalimbali, producers. Hii ilikuwa ni mafanikio makubwa kwani ilionyesha maana halisi ya mtandao.
Pamoja na maelezo ya madhumuni ya kutengeneza mtandao, mwenyekiti wa
Mtandao John Kitime alieleza kuwa wanamuziki wa Tanzania lazima
wafanye kazi ya ziada ili kuwakamata kimaendeleo wenzao wa nchi nyingine Afrika. Wanamuziki
walielezwa umuhimu wa kutumia teknolojia ya internet kwa kuhakikisha kuwa kila
mwanamuziki ana anwani ya barua pepe na kujitahidi kuingia kwenye mitandao ya
kijamii kama Facebook na kuitumia vizuri kwa kutangaza kazi zao. Wanamuziki
walikaribishwa kutumia blog yao ya www.tanzaniamusicians.blogspot.com
kwa kupeleka matangazo, picha za matukio mbalimbali hata ya shughuli binafsi
kama birthday, harusi na kadhalika
na pia kutuma hata nyimbo zao ili ziweze kutundikwa katika mtandao huo bure bila malipo.
Wanamuziki walielekezwa kutuma kazi zao kupitia anwani ya musicnettz@gmail.com.
Katibu Mkuu wa mtandao Abraham Kapinga, alitoa maelezo kuhusu
hali ya ofisi, ambapo wanamuziki walielezwa kuwa ofisi iko Kinondoni karibu na American
Chips, mtaa wa CHADEMA, na kwa vile ndio tumekabidhiwa ofisi, wanamuziki
waliafikiana kukutana hapo na kuifanyia ofisi usafi, jambo ambalo nalo lilionyesha nia ya wanamuziki kulea chama chao. Mwanamuziki Hussein Jumbe
alijitolea viti 4 kwa ajili ya ofisi, jambo ambalo kwa kila hali ni la kutia
moyo kuhusu mwanzo huu wa mtandao.
Mweka hazina wa Mtandao Asha Salvador alitoa taarifa ya
vifaa vya ofisi vilivyonunuliwa vikiwemo viti, meza feni, na stationary.
Maelezo mengine muhimu yaliyotolewa ni kuhusu wanamuziki
kujiunga na chama, na kulipia ada ili kuweza kuendesha ofisi. Fomu za wanachama
ni shilingi 1000/- ada ya mwaka 5,000/- na kiingilio ni shilingi 20,000/-.
Wajumbe walipata muda wa kutoa mawazo na mapendekezo. Mjumbe
mmoja alitoa mapendekezo ya mtandao kuwezesha wanamuziki kutoa maoni yao kuhusu
Rasimu ya Katiba ya nchi na mjumbe mmoja alijitolea kufuatilia
taratibu za kuhakikisha wanamuziki wanashiriki katika jambo hilo muhimu. Mjumbe mwingine alitaka Mtandao uandae
program za elimu ya Management ya Band na hata elimu kwa wanamuziki kujitambua
na hivyo sio kufika mahala kuporomoka baada ya muda mfupi, pia itolewe elimu
kuhusu haki mbalimbali za wanamuziki. Mmoja wa wajumbe alieleza kuwa ametoka
nje ya nchi karibuni alikopata elimu ya vocal training, na hivyo Mtandao uandae
taratibu ili elimu hii iwafikie wanamuziki waimbaji.
Mjumbe mmoja alitoa taadhari kuhusu hali inayoelekea sasa
ambayo inafanya kuweko na uhasama kati ya wanamuziki wa kizazi kipya na wale wa
zamani, badala ya wote kutambuana kuwa ni wanamuziki wanaoweza kufanya kazi
pamoja na kupata mafanikio makubwa zaidi, Mtandao uliombwa uwe chombo cha
kuunganisha wanamuziki wote bila kujali aina ya muziki wa rika.
Swala la vyombo vya utangazaji liliongelewa hasa kuhusu rushwa
iliyokithiri katika vyombo hivi ikawekwa hadharani. Mjumbe mmoja alieleza kuwa
imefikia kuwa inahitajika shilingi milioni moja kuwezesha wimbo kupigwa katika
radio, kwani kuna mgao wa kuanzia mtu anaweka nyimbo kwenye playlist hadi watangazaji wa vipindi mbalimbali kwa ajili ya kupiga muziki na interviews. Ilionekana tatizo hilo lipo hata kwenye radio zinazopiga muziki wa Gospel
ambako tofauti ni bei tu. Ambapo bei ya kupigwa wimbo ni kati ya shilingi alfu 80 hadi laki
moja. Mtandao ulitakiwa ufuatilie utekelezaji wa sheria ya kulipia matumizi ya
muziki katika vyombo vya utangazaji, ambayo ilikuwa ianze kutumika toka 2003.
Wanamuziki walimaliza siku kwa kutumia muda kujaza fomu za uanachama.
No comments:
Post a Comment