Taarifa
zimetufikia kwenye ofisi ya Mtandao wa Wanamuziki Tanzania, kutoka kwa Muumin Mwinjuma 'Kocha' zikieleza kuwa mmoja wanamuziki wake
aliokuwa nao katika safari ya Msumbiji amepata mkasa wa kuibiwa na kuumizwa muda mfupi kabla ya onyesho kumalizika rasmi. Kwa kadri ya maelezo ya Muumini, bendi ilipiga katika
kitongoji cha Nanyupu, ambapo show hiyo ilikuwa ni ya pili katika mahala hapo
baada ya bendi kufanya show ya kwanza siku ya Jumapili tarehe 20 Septemba.
Kitongoji hiki ni makazi ya wachimbaji wa madini ya Ruby ambapo wengi wao ni
Watanzania, pia kuna wenyeji ambao ni Wamsumbiji, Wasenegali na Wanaijeria
kadhaa. Kwa kuwa Watanzania ni wengi, mara baada ya show ya kwanza, wakazi walimuomba aliyeipeleka bendi wakapige
show nyingine, nae hakukataa kwani alikuwa katengeneza pesa vizuri, hivyo bendi
ilikwenda kupiga tena siku ya Alhamisi tarehe 24 Septemba, siku ya Idd. Wakati
wa kupiga wimbo wa mwisho, muimbaji Amina hakuwa na kazi hivyo alishauriana na madansa watangulie kwenye gari. Madansa waliondoka kwa pamoja na kuelekea
kwenye gari lakini Amina ambaye pia ni katibu wa bendi alipanda kwanza jukwaani
kumuaga Muumini. Aliposhuka kwenye jukwaa kuelekea kwenye gari kundi la vijana
wakaanza kumsemesha Kiswahili nae akawa anajisikia kama yuko na ndugu zake.
Vijana wale ghafla wakamvamia na kuanza kumpiga makofi na kumburula na kumpora
mkoba wake uliokuwa na passport yake na ya mpiga drum na fedha za Msumbiji zenye thamani ya 150,000/-. Wenzie walipofika
kumsaidia tayari vibaka wale walikuwa wameshaingia gizani. Na mara moja dansi lilivunjwa ili
kumpeleka mji wa Pemba kwa matibabu.
Bendi
ilifanya maonyesho mengine mawili katika mji wa Pemba na kuona kuna haja ya kurudi kwanza nyumbani ili Amina apone vizuri, wakati wanamuziki wengine wanategemea kurudi nchini wakati wowote, Amina ataendelea kuwa Msumbiji kwa wiki moja zaidi ili apate matibabu zaidi. Pia bendi inakuja kujipanga kwa safari ndefu zaidi
inayotegemewa muda si mrefu.
Amina akiwa na mwanamuziki mwenzie Kupaza |