Shirikisho la Muziki Tanzania ambalo ni muungano wa vyama
vya muziki, jana 9/11/2017, lilifanya
warsha ya kuchambua makubaliano na kampuni ya COGSNET Technologies Ltd ili
kuweka mazingira ya kuingia mkataba na kampuni hiyo kwa shughuli ya kuunda
Database ya wanamuziki Tanzania.
Mkakati huo ambao ulibuniwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na
Michezo Mhe Mwakyembe mwezi mmoja uliopita, uliongozwa na Rais wa Shirikisho hilo Addo
November na Katibu Mkuu John Kitime na hatimae kuweza kufikia hatua ya
kukutanisha viongozi wa vyama vyote na kukubaliana umuhimu wa kazi hiyo.
Uchambuzi ulichukua zaidi ya saa 7 ambapo wawakilishi 32 kutoka vyama vya
muziki 6 walishiriki. Vyama hivyo vilikuwa Chama cha Muziki wa Injili
(CHAMUITA), Chama cha Muziki wa Dansi (CHAMUDATA), Chama cha muziki wa Kizazi
kipya (TUMA), Chama cha muziki wa rumba (CHAMRUTA), Chama cha Muziki wa Disco
(TDMA), Chama cha Madansa (TDA).
Viongozi wa vyama hivi kwa pamoja walichambua makabrasha mbalimbali yatakayowezesha Shirikisho kuingia mkataba wa kuanza kupata idadi na taarifa kamili za wanamuziki na kazi zao nchini Tanzania. Zoezi hili litakapoanza litafanyika nchi nzima na wanamuziki wa aina zote wataingizwa katika Database na hivyo kutoa picha halisi ya shughuli za muziki nchini na pia kusaidia wanamuziki katika namna mbalimbali ikiwemo kuwarahisishia biashara ya kazi zao.
Viongozi wa vyama mbalimbali vya muziki |
Viongozi na wanachama wa vyama vya muziki |