Hii ndio PRESS RELEASE iliyosomwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa
Wanamuziki siku ya 27 August 2014 kwa waandishi wa habari jijini
Dodoma. Ndugu waandishi wa habari, katika mfumo wa sanaa wa nchi
yetu wasanii wamegawanyika katika makundi makuu manne, ambayo yanaendeshwa na
Mashirikisho ya vyama mbalimbali vya sanaa. Mashirikisho hayo ni;
i.
Shirikisho la Filamu TAFF
ii.
Shirikisho la Sanaa za Maonyesho
iii.
Shirikisho la Sanaa za Ufundi
iv.
Shirikisho la Muziki
Tuliopo mbele
yenu ni viongozi na wasanii kutoka vyama na Mashirikisho ya sanaa yaliyotajwa
hapo juu. Kundi hili limekuwepo hapa Dodoma kwa siku mbili kukutana na wajumbe
wa Bunge la katiba ili kufuatilia maslahi ya wasanii katika katika mchakato wa Katiba mpya ya nchi yetu Tanzania. Hii si mara ya kwanza kwa kundi hili
kukutana na Wabunge wa Bunge hili la Katiba, bali hii ni mara ya tatu kundi
hili limefika hapa Dodoma. Mchakato uliotufikisha leo hapa ulianza kwa
Mashirikisho kukutana na kutengeneza Baraza la katiba ambapo mashirikisho
yalitoa mapendekezo kadhaa yaliyofikishwa kwenye Tume ya Katiba. Lakini
hakukuweko jambo lolote lililotokana na mawazo hayo ambalo lilichukuliwa na
kuingizwa kwenye Rasimu ya Katiba. Mashirikisho yalituma majina 36, (tisa
kutoka kila shirikisho) katika
kupendekeza wawakilishi katika Bunge la Katiba. Katika hili mjumbe mmoja,
Paulynus Raymond Mtenda aliteuliwa na hivyo kubeba uwakilish wa kundi zima la
wasanii Tanzania. Siku ya Ijumaa 14/2/2014 Mashirikisho yote ya sanaa
yalikutana BASATA na kumkabidhi rasmi mapendekezo yao Mbunge huyu, ili
ahakikishe kundi hili haliachwi katika mchakato wa Katiba.
Muda mfupi baada ya hapo kundi hili lilikuja Dodoma, na
kukutana na Wabunge mbalimbali wa Bunge hili la Katiba, tulikutana na Wabunge
wa kambi zote na kufanya nao mikutano mingi, ambayo mingine ilifika mpaka saa
nane za usiku. Wabunge wa kambi zote walionekana kuunga mkono hoja za wasanii
na tulianza mawasiliano mbalimbali na Wabunge yakiwemo ya ana kwa ana, simu na
email, Wabunge wakihitaji documentation mbalimbali kuhusiana na mapendekezo
yetu katika Katiba mpya. Katika
kipindi hiki tulikuja wakati hata Mwenyekiti wa Bunde la Katiba hajachaguliwa.
Ujumbe huu ulikuja tena …. Na hii ni mara ya tatu.
Ujumbe huu toka awali ulikuwa na maombi mawili tu.
i.
Wasanii kutambuliwa kama kundi maalumu kama
yalivyotambuliwa makundi ya wakulima wafugaji, wavuvi. Sababu za kutaka
kutambuliwa huku, ni kuwa kundi hili ni kubwa kuliko hata makundi mengine
yaliyotajwa hapo juu. Takwimu za Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2006
zinaonyesha kuwa wasanii nchini walikuwa kiasi cha milioni 6. Leo ni mika
minane imepita na si siri kuwa kundi hili limekuwa na hivyo kukaribia robo ya
Watanzania, si haki kutolitambua.
ii.
Milikibunifu (Intellectual Property) itajwa
rasmi kama moja ya aina za mali zinazohitaji kulindwa katika katika Katiba
Tumekuja pia na mapendekezo ya namna ya kuingiza hoja zetu
hizi zilizosahauliwa, hatujaja na Ibara mpya kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoonekana
kutuhumu katika magazeti ya juzi. Mapendekezo yetu ni kuwa katika Ibara ya 30
iongezwe aya moja tu ya. Na ibara
ya 37 inayoongelea Haki ya ulinzi wa mali, itambue kuwa pamoja na mali
zinazohamishika na zisizohamishika, pia kuna mali isiyoshikika.
Tumepata faraja kubwa kupokelewa na Bunge hili, Na kuweza kuzunguka kwenye kamati 9 kwa
hizi siku mbili kukumbusha mapendekezo yetu haya, ambayo hayabebi tu wasanii
bali pia wavumbuzi wa kiteknolojia, kibailojia, wasomi watafiti, na wananchi
wote kwa ujumla. Pendekezo letu la pili ni muhimu katika kulinda na kuendeleza
uchumi wa Tanzania. Na sisi kama Watanzania tumeona ni muhimu kutumia nafasi
hii adimu kuhakikisha tunatoa mawazo yetu katika Bunge hili kwani tusipotumia
nafasi hii tutakuwa hatukujitendea haki wala kuvitendea haki vizazi vijavyo vya
Tanzania.
SIMON MWAKIFWAMBA-SHIRIKISHOLA FILAMU TANZANIA (TAFF)
JOHN KITIME….MTANDAO WA WANAMUZIKI TANZANIA (TAMUNET)
No comments:
Post a Comment