Wednesday, February 19, 2014

HARAKATI ZA WASANII KUPATA NAFASI KATIKA KATIBA MPYA—3


Kamati ilipata mapokezi ya heshima kubwa kutoka kwa wabunge wa CHADEMA, ambapo Wabunge  sita wa CHADEMA walikaa na kuwasikiliza wawakilishi hawa wa wasanii wakieleza mapendekezo yao katika Katiba kuhusiana na wasanii. Wasanii wana ajenda mbili,




 1. Kundi la wasanii kutajwa katika Katiba kuwa ni kundi rasmi kutokana na ukubwa wa kundi hili nchini, kama yalivyotajwa makundi ya wakulima, wafugaji, wavuvi na kadhalika, pia mchango wake katika ajira ya vijana na ukubwa wa pato linalotokana na kundi hili, ambalo kutokana na kutokutambuliwa linapotea katika mifuko ya watu na kukosesha wasanii na Taifa pato kubwa. 
2. Wasanii walitaka ubunifu ulindwe kwanza kwa ulinzi wa Milikibunifu kutajwa rasmi katika katiba na hivyo kuwezesha sheria bora kutungwa na pia utekelezaji wa ulinzi wa kazi zao uweko kama ilivyo katika mali nyingine za wananchi wengine. Kikao cha saa moja na nusu kilikuwa cha mafanikio na kuwa na faida kwa pande zote mbili.
Wasanii hawakulala mapema kwani walimalizia siku na kuhamia  eneo jingine ambapo walikuwa na kikao na Mheshimiwa Mbunge wa Donge ambae pia ni Mwenyekiti wa Ummoja wa Vijana wa CCM Taifa Mheshimiwa Sadifa, ambapo kikao hicho kiliisha saa saba ya usiku.

HARAKATI ZA WASANII KUPATA NAFASI KATIKA KATIBA MPYA—2

 Ili kuwezesha kufika Dodoma na kuwakilisha mapendekezo yaliyokusanywa na Mashirikisho, Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (TAMUNET), waliwezesha idadi ya wasanii 12 kufika na kuishi Dodoma. Wasanii hao wakiwemo viongozi toka Mashirikisho wameza kufika Dodoma na kuanza kazi mara moja ya kukutana na Wabunge mbalimbali, na kufanya nao mikutano na mazungumzo ya papo kwa popa na kwa kweli mapokezi yamekuwa ya hali ya juu yanayoleta tumaini kubwa kwa  wote waliofika huku. Wasanii waliomo katika msafara huu muhimu kwa tasnia na Taifa ni

1.     Simon Mwakifwamba – Rais, Shirikisho la Filamu (TAFF)

2.     John Kitime – Mwenyekiti, Tanzania Musicians Network (TAMUNET)

3.     Bishop Hiluka – Katibu Mkuu, TAFF

4.     Yobnesh ‘Batuli’ Yusuph –Msanii/FilmProducer

5.     Samwel ‘Braton’ Mbwana –Tanzania Urban Music Association (TUMA)/Music Producer

6.     Paul ‘P Funk’ Matthysse – Mwenyekiti, Tanzania Producers Association/ Producer

7.     Kulwa ‘Dude’ Kikumba – Msanii/ Producer

8.     Abdul Salvador –Katibu Mkuu, Shirikisho la Muziki Tanzania (TMF)

9.     Adrian Nyangamale – Rais, _Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania

10. Mh. Paulynus Raymond Mtendah – Mbunge Bunge la katiba

11. Yvonne Cherie ‘Mona Lisa’ –Msanii

12. Seleman Hamisi- Producer toka Dodoma

13. Ernest Omalla – Mshauri wa TAFF na TAMUNET

Mara baada ya kufika Dodoma Mbunge wa Bunge la Katiba Mh. Maria Sarungi aliwezesha kufanyika kikao cha kwanza kati yake na wasanii ambapo pia Mh. Paul Makonda alikuweko. Mazungumzo yalifanyika ambapo msafara ukaweza kueleza mapendekezo yake kupitia mshauri mtaalam Ernest Omalla na mwanamuziki John Kitime. Mkutano huu wa saa mbili ulikuwa wenye matumaini makubwa.
Msafara ulitoka hapa na kwenda kwenye mkutano mwingine ambapo msafara tena ulitoa maelekezo yake kwa waheshimia Wabunge watatu, Mh Paul Mtanda, Mh.Livingstone na Mh Murtaza Mangungu, na tena mkutano huo ulikuwa ni mzuri wenye mafanikio mazuri sana. Mheshimiwa Mtanda aliahidi atajitahidi kukusanya wajumbe wa kamati ya Ustawi wa Jamii ili kuweza kupata uelewa wa maombi ya wasanii.


Kamati haikuishia hapo kwani jioni Mheshimiwa  Makonda aliiwezesha kundi hili kukutana na wabunge wengine wakiwemo  Mh. Ahmed Salum, Mh. William Mgeja na Mh. Mpina Mbunge wa Kisesa.


Katika hali ya kuonyesha kuwajali wasanii wabunge wa Dar es Salaam waliwafuata wasanii katika Lodge waliofikia na kuwasikiliza lile ambalo walikuwa wakilitaka. Mheshimiwa Idd Azan na Mh. Abbas Mtemvu waliwakilisha wabunge wa Dar es Salaam na kuwa na saa nzima ya kuwasikiliza wasanii hawa katika malengo yao mawili waliyotaka yaingie katika Katiba.

Tuesday, February 18, 2014

HARAKATI ZA WASANII KUPATA NAFASI KATIKA KATIBA MPYA—1

MH. PAULYNUS RAYMOND MTENDA
 Kuna mashirikisho manne ya sanaa nchini ambayo ni Shirikisho la muziki, Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za Ufundi. Ulipotolewa wito wa makundi maalumu kutoa mapendekezo yao katika Katiba Mpya,  Mashirikisho yalikaa kama Kamati za katiba na kuja na mapendekezo kadhaa kwenye katiba, mapendekezo hayo licha ya kupokelewa na Tume ya Katiba hakuna kilichoingizwa katika Rasimu ya Katiba.
Baada ya hapa ndipo wito ukatolewa wa kupendekeza majina ya watu watakaoingia katika Bunge la Katiba, Mashirikisho yote yalipendekeza majina mbalimbali. Hatimae jina la Paulynus Raymond Mtenda lilirudi kama ndie mwakilishi aliyeweza kutoka katika kundi la Watu wenye malengo yanayofanana .
Tarehe 14, February 2014 viongozi wa Mashirikisho walikutana BASATA kumpongeza Mbunge Mteule huyu na kumkabidhi rasmi mapendekezo ambayo yalipelekwa awali kwenye Tume ya Katiba ili aweze kuyapendekeza katika katiba mpya. 
KAIMU KATIBU MTENDAJI WA BASATA AKIMKABIDHI MAPENDEKEZO YA MASHIRIKISHO MBUNGE MTEULE
 
Pamoja na mapendekezo hayo Shirikisho la Filamu TAFF, na Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (TAMUNET), pia walikuja na hoja mbili muhimu nazo ni;
1.     Kutambuliwa kwa wasanii kama ni kundi maalumu katika Katiba, kama yalivyoweza kutambuliwa makundi ya wakulima, wavuvi na wafanyakazi. Sababu kubwa za kuja na hoja hii ni kutokana na ukweli unaopatikana katika tafiti mbalimbali.  Wasanii ni wengi sana, katika ripoti ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati huo ilikuwa kiasi cha milioni sita. Kwa kuwa ni miaka minane sasa imepita toka wakati wa ripoti hiyo kuna kila sababu ya kuamini kuwa kundi hilo limekuwa kubwa zaidi. Sababu nyingine ni ukweli kuwa wasanii wanasababisha ajira kwa kundi kubwa la watu, wakiwemo wafanyakazi wa vyombo vya utangazaji, wafanya kazi katika biashara ya matangazo, wasambazaji, wafanya biashara ndogondogo, (machinga) na wengine wengi waliomo katika mnyororo wa biashara hii ikiwemo, maproducer, mameneja, mafundi mitambo, watayarishaji wa maonyesho na kadhalika. Hivyo sanaa si utamaduni tu bali ni kazi yenye mapato makubwa. Ripoti ya WIPO ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa kazi zitokanazo na Hakimiliki huingiza fedha nyingi zaidi katika uchumi wa Taifa kuliko MADINI, jambo ambalo ni wazi wengi wanaosikia kwa mara ya kwanza hushangaa kwa kuwa kelele za mapato ya Madini ni kubwa sana katika jamii wakati hakuna anaelalamika kuhusu mapato kutokana na hii raslimali ya nchi inayoitwa sanaa. Ripoti hiyo ya WIPO pia ilionyesha kuwa sekta ya Hakimiliki inaajiri watu wengi zaidi kuliko, sekta za Madini, gesi, maji, Ustawi wa Jamii, Afya, Usafirishaji. Hivyo ni sekta ambayo ina umuhimu sana katika uchumi wa Taifa  ikiwa italindwa inavyostahili.
2.     Hoja ya pili ilikuwa kuwekwa rasmi kipengele cha kutambuliwa kwa Miliki Bunifu na kuhakikishiwa ulinzi na uendelezaji wa shughuli za Milikibunifu katika Katiba. Wasanii hutegemea maendeleo yao na uboreshaji wa kazi zao kwa kulindwa kwa Hakimiliki. Lakini ingekuwa ni uchongo wa mawazo kudai ulinzi wa Hakimiliki peke yake. Hivyo lengo ni kupata ulinzi wa Miliki Bunifu ambayo itasababisha kulinda haki za wasanii ,wabunifu, wagunduzi, wanasayansi na wabunifu wa teknolojia mbalimbali. Kuna mifano kila mara hutolewa ambayo inaonyesha nchi kadhaa ambazo wakati nchi hii inapata uhuru, uchumi wa nchi hizo ulikuwa sawa na uchumi wetu, kama vile Malasia, Thailand na Korea Kusini ambazo kutokana na ulinzi  na uendelezaji wenye mipango wa Miliki Bunifu nchi hizo zimewezesha uchumi wao kukua na kuwa katika uchumi bora duniani.
 

Saturday, February 15, 2014

TANZANIA MUSICIANS NETWORK GETS NEW OFFICES

THE NETWORK has shifted to the new offices this week. The shift had long been awaited as the former premisses were not at all conducive to musicians, as the office space was very small and airless most of the time. Musicians and others in the industry are warmly welcome to the new offices



MTANDAO WA MUZIKI TANZANIA WAPATA OFISI MPYA

Baada ya kuwa na ofisi ya muda ambayo ilikuwa katika mazingira magumu kikazi hatimae Mtandao wa Muziki Tanzania umepata ofisi mpya yenye hadhi ya kuitwa ofisi ya wanamuziki. Ofisi hiyo iko katika barabara inayoelekea Mahakama ya Kinondoni, katika jengo la ghorofa lililojengwa kwa matofari ya kuchomwa. Ofisi iko ghorofa ya 3 chumba na 148. Wanamuziki mnakaribishwa kuitumia ofisi hiyo